Njombe, Septemba 25, 2025 – Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa mapato kupitia zao la parachichi, ambalo limeendelea kuwa mkombozi mkubwa wa kiuchumi kwa wakulima wa mkoa huo.
Akizungumza hayo Septemba 25,2025 katika mkutano wa wadau wa kilimo ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya TAHA, Mhe. Mtaka alisisitiza umuhimu wa kuweka mifumo rafiki ya ukusanyaji wa ushuru inayolinda maslahi ya mkulima.
“Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi tengenezeni utaratibu mzuri wa kushughulikia zao la parachichi hasa linapofika getini, Muwe na mfumo wa ukusanyaji wa ushuru usiowakandamiza wakulima bali uwe rafiki na unaolinda thamani ya zao hili muhimu,” alisema Mhe. Mtaka.
Mkutano huo uliofanyika kwa lengo la kuzindua rasmi msimu wa ununuzi wa parachichi mwaka 2025, ambapo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wakiwemo wakulima, wanunuzi, wasafirishaji na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za maendeleo ya kilimo.
Mhe. Mtaka aliwataka viongozi hao wa halmashauri kuwa wabunifu katika kuanzisha vyanzo vya mapato ambavyo haviwaumizi wakulima bali vinaongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.
“Niombe Wakurugenzi wa Halmashauri kuja na mbinu bunifu za kuongeza mapato bila kumuumiza mkulima. Parachichi ni lulu ya Njombe – tusiiuze kwa hasara kwa sababu ya kukosekana kwa utaratibu mzuri,” aliongeza.
Zao la parachichi limekuwa likipata umaarufu mkubwa kwa ndani na nje ya nchi kutokana na ubora wake, na linatajwa kuwa moja ya mazao ya kimkakati ya biashara kwa mkoa wa Njombe. Kupitia mashirikiano ya wadau mbalimbali, wakulima wameweza kupata masoko ya kimataifa na kuongeza kipato cha kaya.
Mkutano huo ulihitimishwa kwa maazimio ya pamoja kutoka kwa wadau, likiwemo azimio la kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao la parachichi kwa manufaa ya taifa
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.