Njombe, Septemba 26, 2025 – Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amekutana na kufanya kikao na timu kutoka makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na wazalishaji wadogo wa umeme kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, kwa lengo la kujadili uwezekano wa kuanzishwa kwa gridi ya umeme ya Mkoa wa Njombe.
Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Mkoa wa Njombe katika kusukuma mbele maendeleo ya nishati, kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo ya vijijini na mijini.
Mhe. Mtaka aliipongeza TANESCO kwa kujitokeza na kuonesha nia ya kushirikiana na wadau wa ndani ya mkoa, hasa wazalishaji wadogo wa umeme, na akasisitiza kuwa serikali ya mkoa ipo tayari kutoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha azma hiyo inatimia.
“Nawashukuru sana kwa kuitikia mwaliko huu, Hii ni hatua muhimu kuelekea kuimarisha miundombinu ya nishati mkoani Njombe. Serikali ya mkoa itatoa ushirikiano wote unaohitajika ili kuona gridi ya umeme ya mkoa inakuwa kweli,” alisema Mhe. Mtaka.
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Njombe aliwahakikishia wazalishaji hao kuwa ofisi yake iko wazi muda wowote kwa ajili ya kupokea hoja, ushauri au kujadili masuala ya maendeleo ya sekta ya nishati katika mkoa huo.
“Lengo letu ni kuona Njombe inakuwa miongoni mwa mikoa yenye mifumo madhubuti ya usambazaji wa umeme. Karibuni ofisini wakati wowote – tuko tayari kufanya kazi kwa karibu nanyi,” alisema Meneja huyo.
Uanzishwaji wa gridi ya umeme ya mkoa unalenga kuongeza ufanisi wa usambazaji wa nishati, kupunguza utegemezi wa vyanzo vya mbali vya umeme, na kutoa fursa kwa wazalishaji wadogo kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa nishati safi na endelevu
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.