Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mh Anthony Mtaka ametoa rai kwa wananchi wa Wilaya ya Makete Mkoani humo kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la Pareto ili kiweze kuwakwamua kiuchumi.
Wito huo ulitolewa katika mkutano wa wadau wa Pareto na Mdau Mkuu Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) uliyofanyika wilayani hapa na kuwajumuisha pia wakulima wadogo wanaojishughulisha na kilimo hicho ambao ni wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Mtaka alisema anayo dhamira ya kuhakikisha wanafufua zao la Pareto ni kuwaunganisha wakulima na sambamba na kuona kwamba wanaondokana na umasikini.
Aidha, Mtaka alisema katika Wilaya ya Makete yenye kata 23, jumla ya kata 21 zenye ukubwa wa hekta 2,800 zinafaa kwa kilimo cha Pareto.
“Mimi nataka wakulima watajirike, Makete inawanufaika wa Tasaf wapatao 4,569 kwa mwaka wanapata sh. 144,000 mimi moyoni mwangu hii haikubaliki, tuunganishe kati ya kaya na kaya katika uzalishaji wa Pareto ili muondokane na umasikini,” alisema Mtaka.
Mwakilishi wa kampuni ya PCT kutoka Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa, Gerald Joseph alisema kuwa malengo yao ni kufikia tani 990 kwa sababu hapo awali uzalishaji wa Pareto ulikuwa unasuasua.
“Mkulima mwenye eka moja tukichukuwa wastani wa uzalishaji kwa kilo 250 za maua makavu na ukizidisha kwa 3, 500 kwa eka akifuata zile kanuni na taratibu bora za kilimo atapata kwa mwaka mmoja kipato cha sh. 8,75,000,” alisema Joseph.
Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mh.Juma Sweda alisema zao la Pareto katika wilaya hiyo lilianza mnamo mwaka 1931 na kuzalishwa ambapo miaka ya 1990 lilianza kuyumba na kudorora.
Nao baadhi ya wakulima akiwemo, Adrian Sanga alisema pamoja na kuhimiza kufufua zao hilo ni vema pia serikali ikaweka mpango wa kujenga kiwanda wilayani humo.
Hata hivyo katika mkutano huo Kampuni ya Pareto (PCT) iligawa miche kwa kaya zaidi ya 267 za wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kufanya zao hilo kuwa ajenda ya Mkoa wa Njombe.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.