Mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa umma yanaendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Idara ya Afya Njombe, yakihusisha jumla ya watumishi 47 waliopokelewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika mwaka wa fedha 2024/25.
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, ambaye amewataka watumishi wapya kutumia fursa hiyo kujifunza na kuzingatia kanuni za utumishi wa umma kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Bi. Omari alisema: “Ninawasihi mtumie nafasi hii kujifunza kwa makini, mzingatie maadili ya kazi na kuwa waadilifu katika kila mtendaji. Serikali imewaamini na kuwapa nafasi hii, hivyo ni wajibu wenu kuhudumia wananchi kwa weledi na uaminifu.”
Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali zinafundishwa na wataalamu kutoka ofisi na taasisi za Serikali. Mada hizo ni pamoja na: Muundo na Majukumu ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma, Wajibu, Haki, Makosa na Adhabu katika Utumishi wa Umma, Elimu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Elimu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF), pamoja na Wajibu wa Vyama vya Wafanyakazi mahali pa kazi. Vilevile washiriki wanapatiwa elimu kuhusu Lishe na VVU/UKIMWI, Mifumo tumizi ya TEHAMA Serikalini, na Mfumo wa Usimamizi na Upimaji wa Utendaji Kazi kwa Watumishi (Watumishi Portal).
Mafunzo haya ni utekelezaji wa Kanuni G.1(8) ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009, inayomtaka Mwajiri kuandaa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wanaoingia Serikalini ili wawe na uelewa wa taratibu, maadili na miiko ya kazi za umma. Kupitia mafunzo hayo, washiriki wanatarajiwa kufahamu dira, dhima na malengo ya taasisi, kujengewa uelewa wa haki na wajibu wao, kutambulishwa majukumu na viwango vya utekelezaji kazi, pamoja na kupewa mbinu za kukabiliana na changamoto za kikazi na kijamii.
Kupokelewa kwa watumishi wapya 47 mkoani Njombe kumeondoa pengo la upungufu wa watumishi lililokuwepo katika Sekretarieti ya Mkoa na Ofisi za Wakuu wa Wilaya, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.