Njombe, 14 Agosti 2025 – Shirika lisilo la kiserikali la IFAD likishirikiana na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi lilitembelea Mkoa wa Njombe na kufika katika ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, kwa lengo la kutambulisha Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi unaotekelezwa nchini Tanzania.
Wawakilishi wa IFAD walieleza kuwa mradi huo una dhumuni la kuboresha sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kupitia matumizi ya mbegu bora na teknolojia za kisasa, kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wafugaji wadogo. Aidha, walisisitiza kuwa mradi huo utajikita pia katika kushirikisha makundi maalum ya jamii, ikiwemo wanawake kwa asilimia 40, vijana 30 na watu wenye ulemavu kwa asilimia 3.
Akizungumza baada ya kupokea ujumbe huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, aliwashukuru wadau hao kwa kuchagua Mkoa wa Njombe kuwa miongoni mwa mikoa ya mfano katika utekelezaji wa mradi. Alisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo kupitia sekta ya maziwa, na kwamba serikali ya mkoa ipo tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha unafanikiwa.
Mradi huu ulianza kutekelezwa mwezi Julai 2025 katika mikoa 8 ya Tanzania Bara na Visiwani mikoa 5, huku Mkoa wa Njombe ukiwa mmoja wa walengwa. Katika mkoa huu, utekelezaji unafanyika kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe na Halmashauri ya Mji wa Njombe ukilenga kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, kuimarisha mifumo ya ushirika na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.