WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu,amesema serikali kwa upande wa sekta ya afya imedhamiria kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba pamoja na bidhaa zingine za afya ili kuondokana na adha ya kuagiza bidhaa nje ya nchi.
Waziri Ummy alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea na kukagua kiwanda cha kutengeneza mipira ya mikono(Gloves)
kilichopo Idofi Halmashauri ya Mji Makàmbako Mkoani Njombe.
"Sasa hivi asilimia 85 ya bidhaa za afya ikiwemo dawa, gloves, vitendanishi na vifaa vingine tunanunua kutoka nje ya nchi kwahiyo unaponunua nje ya nchi kunakuwa na changamoto ya kuchelewa kufika kwa bidhaa, tunatumia fedha za kigeni kuagiza bidhaa za afya na tunachukua bidhaa duni kutoka baadhi ya maeneo"alisema Ummy.
Waziri Ummy alisema lengo la serikali ni kufikia asilimia 50 ya bidhaa zote za Afya ziwe zinanunuliwa ndani ya nchi kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
Alisema serikali ya awamu ya sita itaendelea kutoa fedha ili kutekeleza miradi yote ya maendeleo ya wananchi hususani katika sekta ya afya ambayo ilianzishwa katika serikali ya awamu ya tano.
Aidha Ummy alisema mpaka sasa zaidi ya billion 11 zimetumika kwenye kuendeleza ujenzi wa kiwanda hicho cha mipira ya mikono ambacho mpaka sasa kimefikia asilimia tisini.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai alisema kiwanda hicho cha dawa kimeshaanza kuzalisha ila kinachosubiriwa ni TMDA kutoa ithibati ili bidhaa iweze kuingia sokoni.
"Ukaguzi wa TMDA unategemea vitu vitatu anaweza kukwambia endelea kila kitu kipo sawa au endelea ila rekebisha hiki na hiki au simamisha kwasababu tuna wasi wasi na usalama wa bidhaa yako" alisema Tukai.
Mwenyekiti kamati ya kudumu ya bunge Afya na masuala ya Ukimwi Stanslaus Nyongo,alisema uwekezaji mkubwa ambao Rais Samia Suluhu Hassan anaufanya ni kuwekeza kwenye afya ya binadamu.
"Kuwekeza kwa binadamu ndiyo jambo la msingi na la kwanza na uwekezaji huo hatuwezi kuwekeza kwa kutegemea bidhaa kutoka nje ni mapinduzi makubwa kwa bidhaa zinazotumika zaidi kwenye hospitali kuzalishwa hapa Tanzania"alisema Nyongo.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka alisema kwakuwa serikali inatumia kiasi kikubwa cha fedha kuagiza mipira ya kiume(Condomu)kutoka nje basi kupitia kiwanda hicho kitakuwa kinatengeneza ili kupunguza uagizaji kutoka nje ya nchi.
"Zaidi ya bilioni 10 za kitanzania zinatumia katika kuagiza kondom nje ya nchi kwahiyo tukasema tutumie nafasi ya uwepo wa kiwanda hiki kutengeneza kondomu za kwetu ili tupunguze kuagiza nje ya nchi"alisema Mtaka.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.