Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda leo amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe, ambapo amekagua na kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo. Moja ya miradi muhimu iliyozinduliwa ni nyumba pacha za walimu katika Kata ya Lubonde, mradi ambao unalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu.
Mhe. Prof. Mkenda pia alitembelea na kukagua Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Shaulimoyo, Lugarawa, akieleza kuridhishwa na maendeleo ya chuo hicho katika kuimarisha elimu ya ufundi stadi kwa vijana wa wilaya hiyo. Aidha, aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa madarasa mapya ya Shule ya Sekondari Lugarawa, hatua inayolenga kupanua uwezo wa shule hiyo katika kutoa elimu bora kwa wanafunzi wa eneo hilo.
Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Mkenda aliwapongeza viongozi wa Wilaya ya Ludewa kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo muhimu ya elimu. Aliwashukuru kwa jitihada zao za kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa ufanisi na inakamilika kwa wakati, ili kuwawezesha wananchi kunufaika moja kwa moja.
Mbali na hayo, Waziri Mkenda alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo kwa mkoa wa Njombe, fedha ambazo zinalenga kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na miradi mingine muhimu ya kijamii.
Miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu, hususan maeneo ya vijijini, ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa za elimu bora na maendeleo endelevu.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.