Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Hamad Y. Masauni, amefanya ziara katika mkoa wa Njombe ambapo alikagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya kikosi cha Zimamoto na Polisi. Katika ziara hiyo, Waziri Masauni alitembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi na Kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaloendelea kujengwa mjini Njombe, mradi ambao uko katika hatua za mwisho za kukamilika. Akiwa katika eneo hilo, alieleza kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi, huku akisistiza umuhimu wa kuwa na miundombinu imara kwa ajili ya kuimarisha huduma za zimamoto mkoani humo.
Aidha, Mhe. Masauni alitembelea jengo la polisi la mkoa wa Njombe ambalo limekamilika hivi karibuni. Jengo hilo jipya limejengwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi kwa askari wa polisi pamoja na kuboresha huduma kwa wananchi wa Njombe. Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya usalama ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa vikosi vya usalama.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Zimamoto wa Mkoa wa Njombe, Mrakibu Msaidizi Joel B. Mwakanyasa, mradi wa jengo la ofisi za Zimamoto unatarajiwa kukamilika kwa gharama ya shilingi milioni 700, ambapo tayari asilimia kubwa ya vifaa na rasilimali zimeshatumika. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi michache ijayo. Waziri alitoa wito kwa wahandisi kuhakikisha kuwa wanakamilisha mradi huo kwa ubora unaostahili na ndani ya muda uliopangwa.
Vilevile, jengo la polisi limekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 1.4, na limejengwa kwa viwango vya juu ili kuhakikisha linaendana na mahitaji ya kisasa ya kikosi cha polisi. Waziri alihitimisha ziara yake kwa kuwapongeza wadau wote walioshiriki katika ujenzi wa miradi hiyo muhimu, na akaahidi ushirikiano wa serikali katika kuhakikisha kuwa miradi mingine ya usalama inatekelezwa mkoani Njombe.
Ziara hiyo iliendeshwa chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, aliyeiwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa, akishirikiana na Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Judica Omari, pamoja na Kamati ya Usalama ya Mkoa.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.