Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi leo Oktoba 1, 2022 wilayani Butiama mkoani Mara amezindua rasmi mbio za hiyari za Mwl. Nyerere Marathon ikiwa ni sehemu ya kuenzi, kutangaza na kuhifadhi historia adhimu na adimu ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere
Mbio hizo zimewahusisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi ambapo washiriki wa mbio hizo wamekimbia kupitia njia alizotumia Hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere kwenda Shule na shughuli zake za kila siku akiwa Butiama.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa chimbuko la mbio hizo ni Mpango wa Miaka 10 ya kumuenzi na kutangaza urithi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndani na nje ya Tanzania
“ Mwalimu Nyerere Marathon itakua endelevu na itafanyika kila mwaka hapa Butiama kupitia njia ambazo Baba wa Taifa alizitumia kwenda shule ya Msingi Mwisenge ili kutangaza na kuhifadhi historia adhimu ya Baba wa Taifa” Amesisitiza Balozi Dkt. Pindi Chana.
Ameongeza kuwa uwepo wa mbio hizo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 71 (g) inayoelekeza kuhifadhi maeneo muhimu ya kihistoria hapa nchini yakiwemo ya Mwalimu Nyerere ambayo ni urithi wa utamaduni wa Taifa, vivutio vya Utalii pamoja na Utafiti.
Aidha, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameeleza kuwa mbali na kutangaza urithi na historia, mbio hizo za hiyari ni zao jipya la utalii kupitia michezo vile vile zimelenga kukusanya michango ya fedha za hiyari kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya makumbusho na vituo vya malikale vya kumbukizi ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambavyo vinaratibiwa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania.
Wakati wa mbio hizo za Mwl. Nyerere Marathon 2022, viongozi, wananchi na wadau mbalimbali wamejitokeza kuungana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana na Naibu wake Mhe. Mary Masanja kwenye mbio hizo kumuenzi muasisi wa Taifa la Tanzania kwa vitendo ambapo wakimbiaji wamekimbia Kilomita 22, 13 na Kilomita 4 kuashiria tarehe, mwezi na mwaka aliozaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.