Njombe, 11 Machi 2025 – Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amefungua rasmi mafunzo ya wanawake wajasiriamali kuhusu taratibu, sheria, na kanuni za kufanya biashara katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA). Mafunzo haya yaliyoandaliwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) yanalenga kuwawezesha wanawake kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuzifikisha kwenye masoko ya kikanda na kimataifa.
Katika hotuba yake, Mhe. Mtaka amepongeza TWCC kwa juhudi zake katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kusisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya bidhaa ili kupata masoko ya uhakika. Ameeleza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuimarisha miundombinu kama barabara, reli, viwanja vya ndege, ili kusaidia wafanyabiashara kusafirisha bidhaa kwa urahisi.
Mhe. Mtaka amewataka wajasiriamali wa Mkoa wa Njombe kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo, utalii, na madini ili kuzalisha bidhaa bora zinazoweza kushindana kimataifa. Pia amezitaka taasisi za serikali na sekta binafsi kushirikiana na wafanyabiashara ili kuhakikisha biashara zao zinakua kwa kufuata sheria na taratibu zinazohitajika.
Akihitimisha hotuba yake, amewahimiza washiriki kutumia maarifa watakayopata ili kupanua biashara zao na kunufaika na fursa za AfCFTA. "Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha tunalitumia soko hili kikamilifu kwa manufaa yetu na maendeleo ya Taifa. Natangaza rasmi kuwa mafunzo haya yamefunguliwa," alihitimisha.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.