Njombe, Julai 2025 – Mradi wa Smart Class (Darasa Janja) katika Shule ya Sekondari Mabatini, iliyopo chini ya Halmashauri ya Mji Njombe, umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, hasa kwenye maeneo ya ufundishaji na ujifunzaji.
Mradi huo umeongeza kwa kiwango kikubwa ubora wa elimu kwa kuwezesha walimu kuandaa masomo kwa njia ya kidijitali, huku wanafunzi wakifaidika kwa kupata maarifa kwa urahisi, ubunifu na mvuto zaidi.
Kupitia darasa hilo, walimu sasa wanaandaa vipindi kwa kutumia teknolojia ya kisasa, jambo ambalo limeboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza ufanisi wa utoaji wa maarifa darasani.
Pia, walimu na wanafunzi hupata nyenzo mbalimbali za kujifunzia kutoka maktaba ya TET kupitia mtandao bila gharama yoyote (zero tariff), ikiwa ni pamoja na nukuu za masomo na marejeo ya kitaaluma yanayowasaidia katika kuongeza uelewa wa kina.
Smart Class hiyo hutumika pia kutoa mafunzo ya ndani kwa walimu chini ya Mpango wa Mafunzo Endelevu ya Kazini (INSET), jambo linalowasaidia walimu kuongeza ujuzi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Zaidi ya hayo, mfumo wa ESS (Elimu Sayansi na Teknolojia) hujazwa kwa haraka kupitia matumizi ya TEHAMA, hivyo kupunguza kazi ya mikono na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Matumizi ya vifaa vya TEHAMA pia yameongeza ushirikiano kati ya shule na taasisi mbalimbali, hatua inayochochea maendeleo ya elimu kwa ujumla.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.