Njombe, Tanzania – Katika kuadhimisha Sikukuu ya Eid El-Fitr, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa Mkono wa Eid kwa watoto wanaoishi katika vituo vya kulelea watoto yatima na wale walio katika mazingira hatarishi mkoani Njombe kwa kuwapatia vyakula na vinywaji.
Msaada huo umekabidhiwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, akiwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe, Mhe. Zakaria Mwansansu, kwa niaba ya Rais. Vituo vyote vya kulelea watoto katika mkoa wa Njombe vimenufaika na msaada huu, ambapo zaidi ya watoto 335 wameguswa na upendo wa Rais Samia.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mhe. Mwansansu alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao za msingi, hasa katika nyakati muhimu kama Eid El-Fitr.
"Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha upendo wa dhati kwa watoto hawa kwa kuhakikisha wanapata chakula cha kutosha, vinywaji na mavazi mapya katika sikukuu hii ya Eid. Huu ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuwajali watoto wa Tanzania bila ubaguzi," alisema Mhe. Mwansansu.
Watoto waliopokea msaada huo walionyesha furaha yao kwa shangwe na nderemo, wakisema kuwa hatua hiyo imewafanya kujiona kuwa sehemu ya jamii. Viongozi wa vituo vya kulelea watoto pia walitoa shukrani zao kwa Rais Samia kwa upendo wake na juhudi za kuhakikisha watoto hao wanapata mahitaji muhimu wakati wa sikukuu hii muhimu kwa Waislamu.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.