Shirika lisilo la kiserikali la One Voice Organization kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, limeendesha kampeni ya kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wazazi na walezi. Lengo kuu la kampeni hiyo ni kuwahimiza wazazi kuwalinda watoto wao dhidi ya ukatili wa kijinsia, hususan katika msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Elimu hiyo ilitolewa Desemba 16, 2024, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Ofisi ya Mtaa wa Lunyanywi. Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji Njombe, Vickiana Kiwelu, aliwataka wazazi kuwa waangalifu zaidi wakati wa kipindi cha sikukuu kwa kuhakikisha watoto wanakuwa salama.
"Katika kipindi hiki cha sikukuu, tunapaswa kuwa waangalifu sana kuhusu watoto wetu, hasa tunapopokea wageni nyumbani. Si kila mgeni ana nia njema. Kama unajua nyumba yako ni ndogo na unalazimika kupokea mgeni, mtafutie malazi sehemu nyingine ili kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili. Tuchukue tahadhari kwa sababu baadhi ya ndugu huja na nia ovu," alisema Kiwelu.
Kwa upande wake, Afisa Miradi wa One Voice Organization, Bw. Paul Kapinga, aliwahimiza wananchi kuwa mabalozi wa kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia. Aliwataka kuhakikisha wanazingatia utu na kutojichukulia sheria mkononi pale wanapokutana na changamoto za kijamii.
"Tuwe mabalozi wa kuzuia ukatili wa kijinsia, hususan kwa watoto. Pale mambo magumu yanapojitokeza, ni muhimu kuzingatia utu na taratibu za kisheria badala ya kujichukulia sheria mkononi," alisema Kapinga.
Aidha, Kiwelu aliwataka wazazi wanaoishi katika ndoa zilizovunjika au kutengana kuhakikisha wanatekeleza jukumu lao la kuwahudumia watoto, akibainisha kuwa kumekuwepo na ongezeko la kina mama kufurika kwenye ofisi za serikali kudai matunzo ya watoto wakati ni jukumu la pamoja la wazazi wote wawili.
"Naomba wazazi, hasa wale walio katika ndoa zilizovunjika, wajitahidi kutimiza jukumu la malezi ya watoto wao. Tumeona ongezeko kubwa la kina mama kufika ofisi za serikali kudai matunzo ya watoto, jambo ambalo linaweza kuepukwa kama wazazi watazingatia majukumu yao," alisisitiza Kiwelu.
Elimu hii inalenga kuhakikisha watoto wanakuwa salama wakati wa sikukuu na kuimarisha mshikamano wa familia katika kupinga ukatili wa kijinsia.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.