Mkoa wa Njombe unajiandaa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024. Uchaguzi huu ni fursa muhimu kwa wananchi kuimarisha ushiriki wao katika maamuzi ya maendeleo na usimamizi wa miradi ya kimaendeleo katika ngazi za vijiji na mitaa.
Kwa kauli mbiu, “Serikali Za Mitaa, Sauti Ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi,” mamlaka za uchaguzi mkoani Njombe zimeendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kupiga kura na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye ngazi za mitaa na vijiji.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amethibitisha kuwa maandalizi ya uchaguzi yamekamilika kwa kiasi kikubwa, huku mipango thabiti ya kuimarisha amani na haki ikiwa tayari. Amesema Njombe imejipanga kuzingatia taratibu zote muhimu kwa lengo la kuweka mazingira salama kwa wapiga kura wote.
Katika kuunga mkono jitihada hizi, Mhe. Mtaka amepongeza kampeni za uhamasishaji zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, akisisitiza kuwa wananchi watapata elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu.
Aidha, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kiraia wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uchaguzi huu. Wamehimiza kuwa ni nafasi ya kipekee kwa wananchi kuchagua viongozi wa karibu wenye uwezo wa kushughulikia changamoto za kijamii.
Wananchi wanaotimiza vigezo vya kupiga kura wanaombwa kuchukua hatua za awali za kujitayarisha, ikiwa ni pamoja na kuhakiki taarifa zao za kupiga kura, ili kuepusha usumbufu siku ya uchaguzi.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni tukio muhimu linalotoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi bora watakaoboresha maisha na kuleta maendeleo katika jamii.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.