Njombe, Agosti 1, 2025.
Mkoa wa Njombe umejipanga kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yatakayofanyika kuanzia leo, tarehe 1 hadi 7 Agosti, 2025, kwa kuwafikia wananchi hususan makundi lengwa kama vile wamama wanaonyonyesha, wajawazito, wanafamilia na walezi. Lengo kuu ni kuelimisha, kuhamasisha na kutoa msaada unaohitajika ili kuhakikisha watoto wanapata unyonyeshaji bora katika miezi ya mwanzo ya maisha yao.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: "Thamini unyonyeshaji Weka mazingira wezeshi kwa mama na mtoto".Kaulimbiu hii inalenga kuonesha umuhimu wa ushirikiano wa familia, jamii na mazingira ya kazi katika kuwezesha mama kunyonyesha kwa mafanikio. Mkoa wa Njombe unasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila mtoto anapata maziwa ya mama kwa kipindi kisichopungua miezi sita ya mwanzo ili kumjengea msingi imara wa afya, ukuaji na maendeleo ya akili.
Mkoa wa Njombe umejipanga kuwafikia wananchi kupitia kampeni za elimu ya lishe na afya, mikutano ya hadhara, vipindi vya redio, pamoja na kushirikiana na wadau wa afya katika kuhakikisha ujumbe unafika kwa wakati.
"Lishe ya mwanao ni mafanikio yake," ikumbukwe kwamba, ushirikiano wa kila mmoja katika kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya msingi ya unyonyeshaji bora.
Ili kupata jumbe za kukukumbusha mambo muhimu kuhusu unyonyeshaji na namna bora ya kumsaidia mama anayenyonyesha, jisajili bure kwa kupiga *148*56*100# na fuata maelekezo. Iwapo usajili haujakamilika, piga tena *148*56*100# kuendelea ulipoishia. Huduma hii inapatikana kupitia mitandao ya Vodacom, Yas, na Airtel Bure.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.