Na. Chrispin Kalinga - Njombe
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya ziara mkoani Njombe ambapo hapo atakuwa na ziara ya siku mbili kuanzia leo tarehe 21 na kesho tarehe 22 Februari 2024, katika ziara hiyo Mhe. Biteko amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka.
Mhe. Biteko wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Wanging'ombe amesema serikali ya awamu ya 6 inaendelea kuifungua Wilaya ya Wanging'ombe ikiwa vijiji vyote 108 vya Wilaya ya Wanging’ombe vimekwishafikishiwa nishati ya umeme kupitia miradi inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo kwa wilaya ya wanging'ombe Serikali imetumia shilingi bilioni 9.5 kupeleka umeme.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Dkt. Festo Dugange, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati na REA kwa kuvifikishia umeme vijiji vyote 108 vya jimbo lake la uchaguzi.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema kuwa kwa sasa REA inatekeleza jumla ya miradi mitatu katika maeneo tofauti ya Wilaya ya Wanging’ombe ikiwa ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B pamoja na Mradi wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.
Katika Hatua nyingine Mhe. Biteko ametembelea Kiwanda cha Kuzalisha Nguzo cha TANWAT, amezindua mradi wa Umeme shule ya sekondari ya wasichana iliyopo wilaya ya Wanging'ombe na mwisho amemaliza ziara yake kwa siku ya leo kwa kukutana na wazalishaji wadogo wa umeme waliokaa kikao katika ukumbi wa mikutano wa Hilside Hotel Njombe.
Ziara hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Ndugu Deo Kasenyenda Sanga.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.