Maafisa Elimu, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa shule za sekondari, na Walimu wa Tarafa ya Njombe Mjini wameonesha kuridhishwa na Mtaala Mpya wa Elimu kwa shule za msingi na sekondari. Wameeleza kuwa mtaala huo umebeba dira ya kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujitegemea kwa kuwawezesha kupata stadi na fani mbalimbali wakiwa shuleni, hatua ambayo itasaidia kupunguza utegemezi wa ajira rasmi pindi watakapohitimu masomo yao.
Kauli hizo zilitolewa wakati wa semina elekezi iliyoandaliwa na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Njombe, Mwl. Prochesusi Jerome Mguli, ambapo Wathibiti Ubora wa shule walitoa mada mbalimbali, wakiongozwa na Bw. Evaristo Maicko Chaula ambaye ni Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule wa Halmashauri hiyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliwahi kusema kuwa mtaala mpya umeanza kutumika rasmi mwaka huu katika ngazi za shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu, na unalenga kumwezesha mwanafunzi kupata elimu inayozingatia ujuzi wa vitendo. “Mtoto akihitimu, awe na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa kwa ujuzi alioupata shuleni,” alieleza Prof. Mkenda. Alliongeza kuwa mtaala huu ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, ambayo inataka elimu ya lazima iwe miaka 10 ili kuhakikisha kila mtoto anamaliza hadi kidato cha nne.
Aidha, mtaala mpya umejumuisha masomo ya amali kama kilimo, ushonaji, useremala, umeme wa majumbani, teknolojia ya habari (TEHAMA) na ufundi stadi, kwa lengo la kuwapa wanafunzi maarifa ya kujitegemea hata kabla ya kuhitimu elimu ya juu. Kupitia mabadiliko haya, Serikali inalenga kutoa wahitimu watakaoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya taifa.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.