Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amesema kuwa uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, hususan parachichi, ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati wa ziara yake katika kiwanda cha kuchakata mafuta ya parachichi kinachomilikiwa na Muricado Fruit Supplies, Mhe. Mtaka alieleza kuwa uwekezaji wa aina hii unatoa fursa kwa wakulima kupata masoko ya uhakika, kuongeza ajira na kuinua pato la taifa.
"Wawekezaji hawa wameamua kuchukua hatua ya kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yetu. Hili ni jambo la kuigwa na linapaswa kuungwa mkono kwa kuwa linachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii," alisema Mhe. Mtaka.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira bora kwa wawekezaji kwa kuboresha miundombinu, upatikanaji wa umeme na sera zinazowiana na maendeleo ya viwanda.
Aidha, aliwahimiza wakulima wa parachichi kuongeza uzalishaji wao kwa kufuata mbinu bora za kilimo, kwani mahitaji ya bidhaa zinazotokana na parachichi yanaongezeka katika soko la kimataifa.
Mhe. Mtaka alihitimisha kwa kusema kuwa Mkoa wa Njombe unaendelea kuwa kinara katika kilimo cha parachichi, na kwamba juhudi za wawekezaji katika sekta hiyo zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote ili kufanikisha azma ya Tanzania ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.