Zaidi ya malori mia mbili ya mazao ya misitu mkoani Njombe yamekwama kutokana na kukwama kwa mfumo wa malipo ya tozo za vibali vya usafirishaji wa mazao ya misitu kwa zaidi ya wiki moja.
Wakizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka leo wafanyabiashara hao walisema Julai mwaka huu kuelekea mwaka mwingine wa fedha malori hayo.yalikwama kusafirisha mbao kwa muda wa wiki moja na baadae kuruhusiwa baada ya kutolewa kwa malalamiko na wafanyabiashara hao.
Walisema licha ya kukatiwa ushuru lakini baada ya kufuatilia kibali cha kusafirisha mbao kinachotolewa na Wakala wa Misitu mkoani Njombe wakaambiwa mfumo unasumbua hivyo kusababisha kupaki malori kwa muda mrefu licha ya kuwa na mzigo.
Walisema na safari hii jambo hilo limejirudia tena ambapo zaidi ya wiki sasa malori ya kusafirisha mbao yamekwama kutokana na kile kinachodaiwa kukwama kwa mfumo wa vibali vya kusafirisha misitu.
Walisema biashara wanayoifanya inategemea mikopo kutoka taasisi za fedha hivyo wanavyoendelea kusubiri mfumo ukae sawa marejesho yanahitajika hivyo wanapata wakati mgumu.
Walisema kukwama kwa malori hayo kwa muda mrefu kuna sababisha kupungua kwa uaminifu kwa wateja wao ambao wamekuwa wakifanya biashara nao kutokana kuchelewesha bidhaa zao.
Baadhi ya wafanyabiashara hao wakiwemo Sophia Raymond na Subira Kyando waliiomba serikali kupunguza vituo vya ukaguzi wa mazao ya misitu kwani vimekuwa vikileta usumbufu kwa kuchukua muda mrefu wa safari.
"Hii faini ambayo maliasili yamekuwa wakiwapiga madereva sababu ya kuruka kituo bila kukaguliwa ni uonevu kwasababu madereva wengine ni wageni hivyo kuwe na vituo vichache vitakavyotambulika kwa urahisi" alisema Raymond.
Wakala wa Misitu mkoa wa Njombe Audatus Kashamakula alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kudai kuwa imetokana na kusimama kwa mifumo ya utozaji kodi ya Wizara ya Fedha jambo ambalo lipo nje ya uwezo wao kwasasa.
Alisema wamekuwa wakijitahidi kutoa huduma hata muda wa ziada ili kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika utoaji wa vibali.
"Nipende kuwaomba radhi wadau wetu wa mazao ya misitu wasafirishaji na madereva kwa hili ambalo limetokea na tutafanyia kazi changamoto zote ambazo zimetokea hasa mfumo ambao ulikuwa haujakaa sawa" alisema Kashamakula.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka aliziomba wizara zinazohusika kushughulikia tatizo hilo haraka ili kunusuru mapato ya mkoa huo ambayo zaidi ya asilimia sabini yanategemea mazao ya misitu.
Alisema uchumi wa mkoa wa Njombe zaidi ya asilimia sabini unategemea mazao yatokanayo na misitu hivyo lazima kuwepo na usimamizi utakaoweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu.
"Mbao inabeba zaidi ya asilimia sitini hadi sabini ya uchumi wa mkoa hivyo tunao wajibu wa kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya biashara kuliko kuwaza kukusanya tu" alisema Mtaka
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.