Mkurugenzi wa Kiwanda cha Muricado Fruit Supplies, Josiah Mrimi, ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji mkoani Njombe, hatua inayowezesha sekta ya viwanda kuendelea kukua na kuleta maendeleo kwa wakulima na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Mkurugenzi huyo alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, kwa juhudi zake za kuvutia wawekezaji na kuhakikisha miundombinu muhimu inafikishwa kwenye maeneo ya uwekezaji.
"Tunatoa shukrani za dhati kwa Serikali, hususan kwa uongozi wa Mkoa wa Njombe chini ya Mhe. Anthony Mtaka, kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji. Kupitia juhudi zake, tumeshuhudia uboreshaji wa barabara, upatikanaji wa umeme wa uhakika, maji na hata huduma za mawasiliano, mambo ambayo yamewezesha sisi na wawekezaji wengine kuendesha shughuli zetu kwa ufanisi," alisema Mrimi.
Aliongeza kuwa uwepo wa miundombinu hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha shughuli za kiwanda chake, ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa malighafi na bidhaa za mwisho kwenda kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
"Tunaamini kuwa jitihada hizi za serikali zitaendelea na zitawahamasisha wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa Njombe, hususan katika sekta ya viwanda vya kuongeza thamani ya mazao," aliongeza.
Mrimi aliwahakikishia wakulima wa parachichi kuwa kiwanda hicho kimejipanga kuwapa soko la uhakika, huku akiomba Serikali kuendelea kushirikiana na wawekezaji wa ndani ili kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.