Na. Chrispin Kalinga - Ludewa, Njombe
Ludewa, Njombe – Septemba 26, 2024 – Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Ndugu Sunday Deogratias, jana alifanya mkutano muhimu na viongozi wa dini pamoja na viongozi wa vyama vya siasa kujadili maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano huo, Ndugu Deogratias alisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini na siasa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uwazi, na haki. Alieleza kuwa mchango wa viongozi hao katika kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu ni wa msingi kwa maendeleo ya demokrasia na ustawi wa jamii katika wilaya ya Ludewa.
“NINAWAOMBA VIONGOZI WA DINI NA VYAMA VYA SIASA KUWAHAMASISHA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KATIKA MCHAKATO WA UCHAGUZI, KICHUKUE FOMU NA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA. UCHAGUZI HUU NI FURSA YA KUJENGA SERIKALI ZA KIUWAJIBIKAJI NA ZENYE KUZINGATIA MAENDELEO YA WANANCHI,” alisema Deogratias.
Pia, Ndugu Deogratias alieleza kuwa serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa njia ya haki, huku akisisitiza kuwa vyama vya siasa vina wajibu wa kuepuka vurugu na maneno ya uchochezi. Aliongeza kuwa ni muhimu kila mgombea na chama kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa ili kulinda amani wakati wa uchaguzi.
Kwa upande wa viongozi wa dini, waliombwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii zinaendelea kuwa na utulivu, hususan katika kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi. “VIONGOZI WA DINI MNA NAFASI YA KIPEKEE KATIKA KUWAONGOZA WANANCHI KUSIMAMA KATIKA ZILIZO SAHIHI, KUWEKA MBELE AMANI NA MAENDELEO YA JAMII YETU,” aliongeza.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka madhehebu mbalimbali pamoja na viongozi wa vyama vya siasa ambao walitoa michango yao kuhusu namna bora ya kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanikiwa na kutoa viongozi watakaowajibika kwa wananchi.
Mwisho, Ndugu Deogratias aliwataka wananchi wa Ludewa kushiriki kwa wingi katika mchakato wa uchaguzi kwa kujiandikisha, kuchukua fomu za kugombea, na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili sauti yao isikike na kuchangia maendeleo ya jamii.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.