Njombe, Desemba 13, 2024 – Uongozi wa Kampuni ya Avocado Avenue Tanzania Ltd ukiongozwa na Bw. Amin Manji, leo umefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe na kupokewa rasmi na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Anthony Mtaka.
Katika mazungumzo yao, walijadili masuala muhimu yanayolenga kuimarisha uchumi wa wakulima wa parachichi mkoani Njombe. Miongoni mwa mambo yaliyopatiwa msisitizo ni kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata parachichi ambacho pia kitatengeneza mafuta ya parachichi. Aidha, kampuni hiyo imeahidi kununua parachichi zote, ikiwemo zile zilizokataliwa, na kuzigeuza kuwa bidhaa mbalimbali kwa ajili ya masoko ya ndani na ya kimataifa.
Mbali na kiwanda, Avocado Avenue Tanzania Ltd imeeleza mipango yao ya kutoa soko endelevu la parachichi kwa wakulima wa Njombe. Kampuni hiyo pia imeahidi kutekeleza programu za kuwawezesha wakulima kwa:
Kutoa maarifa ya kitaalamu kuhusu kilimo bora cha parachichi.
Kutoa msaada wa utunzaji wa mazao.
Kuwasaidia wakulima kufanikisha mavuno bora na kuendeleza kilimo endelevu.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi Machi 2025, ambapo kampuni hiyo itaanza kupokea mazao ya parachichi kutoka kwa wakulima. Aidha, kiwanda hicho kitatoa ajira za kudumu kwa watu 100 na ajira za mikataba kwa takriban watu 300, huku wakitarajia kushirikiana na kuwafikia zaidi ya wakulima 1,500.
Mhe. Anthony Mtaka ameipongeza Avocado Avenue Tanzania Ltd kwa kuamua kuwekeza mkoani Njombe. Akizungumza wakati wa kikao hicho, alisema:
“Nawashukuru sana kwa kuja kuwekeza katika sekta ya parachichi mkoani Njombe. Uamuzi wa kujenga kiwanda cha kuchakata parachichi hapa Njombe utaongeza thamani ya tunda hili moja kwa moja kuanzia hapa hapa mkoani. Hatua hii itakuza uchumi wa wakulima wetu na kuongeza ajira kwa wananchi wa Njombe na maeneo ya jirani.”
Kampuni ya Avocado Avenue Tanzania Ltd imeonyesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na mkoa wa Njombe kuimarisha sekta ya kilimo cha parachichi na kuboresha maisha ya wakulima.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.