Mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Anthony Mtaka amesema Mkoa wa Njombe una mahitaji ya mbolea zaidi ya Tani 112 lakini mpaka sasa lengo hilo halijafikiwa. Amesema uwepo wa kampuni ya mbolea hiyo unatoa fursa kubwa kwa wakulima wa Mkoa huo katika kuongeza tija na kipato kwenye maeneo hayo.
"Tunaipongeza sana Intracom kwa uwamuzi wake muhimu na mzuri katika nyanda za juu kusini kwani mbolea hii itaongeza tija na kipato kwa wakulima" amesema Sweda.
Mkurugenzi Mtendaji kampuni ya Mbolea ya Intracom Nazaire Nduwimana amesema kiwanda hicho kupitia mbolea ya FOMI kina mchango mkubwa katika mapinduzi ya kilimo hapa nchini.
"Huwezi kuzungumza kilimo bila ya kutaja mbolea na mbolea inayohitajika ni ile iliyosahihi na inayoweza kumkomboa mkulima na kuinua kipato chake na kukuza uchumi" amesema Nduwimana.
Meneja Mkuu wa kampuni ya mbolea ya Mtewele Traders iliyopo mkoani Njombe Sady Mwang'onda amesema uchakachuaji wa mbolea mara nyingi hutokea pindi bidhaa hiyo inapokuwa adimu hivyo uwepo wa mbolea ya Fomi unakuja kupunguza changamoto ya mbolea kwa wakulima na kuondoa kabisa uchakachuaji.
"Uchakachuaji wa mbolea mara nyingi hutokea pindi bidhaa inapokuwa adimu kwahiyo upatikanaji wa mbolea za kutosha unakwenda kuondoa uchakachuaji kwasababu mbolea zitakuwa zinapatikana kwa wingi" amesema Mwang'onda.
Nao wakulima Mkoani Njombe wameiomba serikali kuwadhibiti mawakala wa mbolea wasiowaaminifu ambao wanachakachua mbolea na kusababisha hasara kubwa kwao.Hii ni baada ya msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 baadhi ya wakulima kuuziwa mbolea iliyochanganywa na mchanga na kusababisha hasara kubwa kwao.
Ombi hilo wamelitoa leo kwenye mkutano wa wadau wa Kilimo Nyanda za juu kusini ulioandaliwa na Kampuni ya mbolea ya INTRACOM na kufanyika mkoani Njombe.Wamesema mawakala wenye tabia za kuchakachua mbolea wanatakiwa kupewa adhabu kubwa ili kutoa fundisho kwa wengine wenye tabia hizo.
Wamesema mwaka jana mkoa wa Njombe umepata kashfa kubwa ya uchakachuaji wa mbolea kwa kuweka mchanga na msimu wa kilimo umeanza serikali inatakiwa kuwadhibiti mawakala wasio waaminifu ili kulinda maslahi ya wakulima mkoani Njombe.
Baadhi ya wakulima hao akiwemo Frank Mwenda amesema Mawakala wa Mbolea wanatakiwa kuepuka kuingia kwenye mkumbo wa kuuza mbolea iliyochakachuliwa kama ilivyofanywa na wenzao katika msimu wa kilimo uliopita.
"Kwahiyo serikali isimamie zaidi na watu wanaochakachua mbolea wapate adhabu kubwa ili kuwa mfano kwa wengine ili wasiweze kufanya hivyo" amesema Mwenda.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.