Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka ametoa rai kwa wafanyakazi wa makampuni na wazalishaji wa mbolea nchini kuepuka udanganyifu na uchakachuaji wa mbolea hali inayoumiza wakulima na kutia hasara Taifa.
Mtaka ameyasema hayo mara baada ya kuzindua ghala la kuhifadhia mbolea za kampuni ya ITRACOM ya Mkoani hapa,alisema msimu wa kilimo iliyoisha kumefanyika sana vitendo vya udanganyifu.
‘’Kampuni moja sitaki kuitaja jina kwa sababu ya biashara hapa Njombe,msimamizi wa ghala alifanya mchezo kwenye akawa anapaki mbolea aina hiyo anaweka mchanga,mteja anajua ni mbolea imefungwa kumbe ni mchanga, lakini tulipata wasimamizi wa magodaun wanafanya michezo na wafanyabiashara ambao sio waaminifu’’alisema.
Mtaka alisema‘’mfuko umepimwa kilo 25 unapunguzwa kilo nne inabaki 21,mfuko ni kilo 50 anatoa tano inabaki 45,anachukua mchanga mweupe,anasaga chumvi anachanganya hadi mchele kwenye mbolea’’
Mtaka ametoa wito kwa wasimamizi wa maghala kuwa waaminifu na kuacha michezo michafu kwa sababu ya kuchukua mchanga na kwenda kuweka kwenye maghala ili kuonekana kwamba mbolea ipo nyingi.
Hata hivyo Mtaka ameongeza kuwa mahitaji ya mbolea kwa sasa mkoa wa Njombe ni tani 112,000 na kutoa wito kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya kuwekeza ili wakulima wasikose mbolea.
Mawakala wadogo wa pembejeo mkoa wa Njombe akiwemo Olaph Mhema waliomba mbolea zinazozalishwa nchini zipunguzwe bei na kusambazwa kwa wakati.
‘’Mbolea za Intracom bado zipo bei kubwa sana,wanazalisha kilo 25 hawana kilo 50 lakini bado inagharama kubwa sana kwa hiyo haiwezi kushindana na mbolea za nje,kiwanda ni cha kwetu kama wanakwama kwenye uzalishaji serikali muingilie kati’’alisema.
Nae Mkurugenzi wa Biashara na Masoko Itracom Dk. Keneth Masuki alisema mbolea hiyo tayari imeshambazwa zaidi ya mikoa Kumi na Nane ambapo kwa msimu uliopita mbolea aina Tatu zimezalishwa zikiwemo Fomi otesha, Fomi kuzia na Fomi nenepesha.
‘’Mkakati wa usambazaji wa mbolea zetu kwa msimu uliopita tulifika mikoa karibu 18,sasa hivi tumeona tufungue maghala baadhi kwa kuanzia ili mbolea iwe karibu na wateja wadogo wadogo,mawakala ambao hawawezi kuchukua lori zima’’alisema Masuki.
|
|
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.