Njombe, 14 Januari 2025 - Christian Social Services Commission (CSSC), taasisi ya kiekumene iliyoanzishwa mwaka 1992 na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) pamoja na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), imetembelea ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe kwa lengo la kutambulisha mradi wa Global Fund.
Mradi huo unatekelezwa chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya, ukilenga afua za vijana, hususan wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW), ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI. Shirika la TAYOA limepewa jukumu la kutekeleza mradi huo kwa kipindi cha mpito kuanzia Desemba 2024 hadi Machi 2025.
Watekelezaji wa Mradi huo ukiongozwa na Meneja wa Kanda ya Kusini, Fr. Manfred Mjengwa, walipokelewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Zakalia Mwita. Katika kikao hicho, viongozi wa CSSC walieleza dhamira yao ya kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii kupitia mradi huu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Mwita alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kama CSSC katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi. Alibainisha kuwa mradi huu ni hatua muhimu katika kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana, kuboresha huduma za kijamii, na kupunguza maambukizi ya VVU na UKIMWI mkoani Njombe.
Kwa upande wa, CSSC waliahidi kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakuwa endelevu kwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wa mkoa, wa wilaya, na wananchi wa Njombe. Aidha, walisisitiza kuwa mradi huu unalenga kuleta maendeleo kwa jamii kwa kuhakikisha huduma bora za afya na ustawi wa kijamii zinawafikia walengwa.
Mradi wa Global Fund unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa vijana wa Njombe, huku ukiboresha ustawi wa kijamii na kupunguza changamoto za afya zinazowakabili wananchi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.