Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, alishiriki katika zoezi la kupiga kura kwa kupiga kura yake katika kituo cha Lunyanywi, Halmashauri ya Mji wa Njombe. Akizungumza baada ya kupiga kura, Bi. Omari amewapongeza wananchi waliojitokeza mapema na kuwasihi waliobaki kuitumia fursa hii ya kidemokrasia kabla ya muda wa upigaji kura kuhitimishwa.
"Ni muhimu kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura ajitokeze kushiriki. Hii ni nafasi pekee ya kuhakikisha tunachagua viongozi bora wa mitaa na vijiji ambao wataongoza maendeleo yetu kwa miaka ijayo," alisema Bi. Omari.
Aidha, Katibu Tawala huyo ameeleza kuwa vituo vya kupigia kura mkoani Njombe vipo katika hali ya utulivu, akisisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kuamini mchakato huu. "Mazingira ya upigaji kura ni salama na tulivu. Hakuna sababu ya kusita. Kila mmoja ajitokeze haraka kabla ya muda wa kufunga vituo kufika," aliongeza.
Wananchi wapatao 457,317, sawa na asilimia 86 ya waliojiandikisha, wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa. Bi. Omari amesisitiza kuwa ushiriki wa kila mmoja unahitajika ili kuhakikisha maendeleo ya Njombe yanakuwa shirikishi na yanayoendana na mahitaji ya wananchi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.