Na. Chrispin Kalinga - Njombe
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Pembejeo, Bi Mwanahiba Mzee, ametoa wito kwa vijana wa Mkoa wa Njombe kuchangamkia fursa za mikopo ya kilimo inayotolewa na Taasisi hiyo, akisisitiza kuwa kilimo ni sekta yenye uwezo wa kuinua uchumi wa vijana na jamii kwa ujumla. Mkurugenzi alitoa rai hiyo wakati wa kikao kilichohudhuriwa na vijana na Wanawake wa Wilaya ya Njombe, kikao ambacho kiliendeshwa chini ya uongozi wa Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa.
Akizungumza na washiriki wa kikao hicho, Bi. Mwanahiba alieleza kuwa mikopo hiyo inalenga kuwasaidia vijana na Wanawake kuanzisha na kuendeleza miradi ya kilimo, ikiwa ni moja ya juhudi za Taasisi hiyo chini ya Wizara ya Kilimo katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa vijana na wanawake katika kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira.
"Tunaamini kuwa kilimo kina uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya vijana na Wanawake, na fursa za mikopo hii ni njia mojawapo ya kuwawezesha kufikia mafanikio. Nawahimiza vijana na Wanawake wote wa mkoa wa Njombe kuchangamkia fursa hii ili waweze kujijenga kiuchumi kupitia kilimo," alisema Mkurugenzi.
Aliongeza kuwa vijana wanahitaji kubadili mtazamo wao juu ya kilimo, akibainisha kuwa sekta hii sasa inahitaji ubunifu na teknolojia mpya ili kuongeza uzalishaji na tija.
"Kilimo siyo kazi ya kizamani; sasa hivi tunalenga kilimo cha kisasa kinachotumia teknolojia bora. Vijana wana nafasi kubwa ya kuleta mapinduzi ya kilimo hapa Njombe," alieleza Mkurugenzi.
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa, aliunga mkono kauli hiyo na kuwaomba vijana kuchukua hatua za haraka katika kutumia mikopo hiyo ili waweze kujikwamua kiuchumi. Aliwahakikishia kuwa serikali inawaunga mkono kwa kuhakikisha mazingira bora ya kilimo yanakuwepo, pamoja na kuweka mipango ya kuwawezesha wakulima wadogo wadogo.
"Mikopo hii ni fursa nzuri kwenu vijana. Tunawaomba muwe mstari wa mbele kutumia nafasi hii kwa maendeleo yenu na ya jamii nzima. Ni wakati wa kuchukua hatua na kujenga maisha bora kupitia kilimo," alihimiza Mhe. Gwakisa.
Kikao hiki kilipata mwitikio mzuri kutoka kwa vijana, wengi wakionesha nia ya kujiunga na mpango wa mikopo ili kuanza safari ya kujiajiri kupitia kilimo.
Mfuko wa Pembejeo ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Kilimo inayolenga kuondoa changamoto kwa wakulima wadogo kupata pembejeo za kilimo kwa gharama na masharti nafuu. Mfuko wa Pembejeo unatoa mikopo ya kilimo kwa riba ya asilimia 4.5 kwa ajili ya vijana na Wanawake, na riba ya asilimia 6 hadi 7 kwa wanaume waliozidi miaka 40.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.