Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) umeanzisha mpango wa kugawa mitungi 13,020 ya gesi katika wilaya nne za mkoa wa Njombe. Kila wilaya itapokea mitungi 3,255, ambayo itauzwa kwa nusu bei, huku nusu nyingine ya gharama ikigharamiwa na serikali.
Akizungumza wakati wa kutambulisha mpango huu leo, tarehe 19 Novemba 2024, katika ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage, alisema kuwa lengo kuu ni kupunguza gharama kubwa ambazo wananchi wamekuwa wakilalamikia. “Serikali imeamua kulipa nusu ya gharama ili kupunguza mzigo kwa wananchi,” alisema Mhandisi Advera.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwijage, mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na kampuni ya Taifa Gas, ambayo imesaini mkataba mnamo mwezi wa Septemba mwaka huu. Gharama jumla ya mradi ni shilingi milioni 254, ambapo Taifa Gas itahudumia mkoa wa Njombe kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Wananchi watatakiwa kuonyesha vitambulisho vya taifa ili kufaidika na punguzo hili, na kila mtungi utauzwa kwa shilingi 19,500. Tathmini ya awali itafanyika baada ya usambazaji ili kutathmini kama wanufaika wataendelea kutumia gesi baada ya matumizi ya awali.
Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, Mkuu wa Idara ya Miundombinu, Mhandisi Rutashibilwa, alisisitiza umuhimu wa elimu kuhusu faida za nishati safi. “Njombe inakutana na changamoto kubwa kuhusu matumizi ya kuni na mkaa, lakini kupitia mpango huu, tuna matumaini kwamba tutaweza kupiga hatua kubwa katika kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi,” aliongeza.
Mpango huu ni sehemu ya jitihada za serikali kupunguza uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba, kutunza mazingira, na kukuza matumizi endelevu ya nishati safi katika kaya za vijijini.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.