Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amepongezwa kwa juhudi zake za kusuluhisha mgogoro uliodumu kwa muda kati ya viongozi wa Chama cha Ushirika Msowelo na wanachama wake. Mgogoro huo ulikuwa umesababisha mkwamo katika utekelezaji wa majukumu ya chama hicho, lakini sasa umefikia tamati.
Akizungumza katika mkutano wa maridhiano uliofanyika jana tarehe 22 Novemba 2024 kŵenye ofisi ya chama cha ushirika huo , Mhe. Mtaka amewataka viongozi wa Chama cha Msowelo kuzingatia mshikamano na uadilifu katika kusimamia maendeleo ya chama hicho. Alieleza kuwa ushirikiano wa dhati baina ya viongozi na wanachama ni nyenzo muhimu ya kuimarisha uchumi wa wanachama na jamii kwa ujumla.
“Natoa wito kwenu kuacha tofauti za kikundi au binafsi na kujikita zaidi katika maendeleo ya chama na ustawi wa wanachama wenu. Ushirika unapaswa kuwa mfano wa mshikamano na usawa,” alisema Mhe. Mtaka.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alitumia jukwaa hilo kuwakumbusha wananchi wa Mkoa wa Njombe kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024. Alisisitiza kuwa uchaguzi huo ni fursa muhimu ya wananchi kuamua viongozi wanaotakiwa kuongoza maeneo yao kwa maslahi ya umma.
“Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha tunajitokeza kupiga kura. Serikali za mitaa ni sauti ya wananchi, na ushiriki wenu ndiyo msingi wa maendeleo ya demokrasia,” aliongeza.
Wanachama wa Chama cha Msowelo walielezea kuridhika kwao na juhudi za Mkuu wa Mkoa katika kumaliza mgogoro wao uliopelekea kushindwa kuanza shughuli yao ya kilimo kwa wakati, wakiahidi kuendelea kushirikiana kwa manufaa ya chama na jamii kwa ujumla.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.