Njombe –Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu Mkoa wa Njombe, Bw. Lewis Mnyambwa, amewataka Wakuu wa Idara mkoani humo kuzingatia kwa makini sheria za manunuzi ya umma na kuhakikisha tenda zote za serikali zinatangazwa na kushughulikiwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa National e-Procurement System of Tanzania (NeST), kama ilivyoelekezwa na mamlaka husika.
Akifungua semina elekezi ya mafunzo ya sheria na matumizi ya mfumo wa ununuzi wa umma (NeST), yanayoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa siku tano katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Mnyambwa alisisitiza kuwa kutofuata masharti ya sheria hiyo kutachukuliwa kama uvunjifu wa taratibu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika.
“Ni wajibu wa kila kiongozi wa idara kuhakikisha taratibu za manunuzi ya umma zinafuatwa ipasavyo. Mfumo wa NeST umeanzishwa kwa lengo la kuongeza uwazi, kuondoa mianya ya rushwa, na kuhakikisha thamani ya fedha za umma inapatikana. Hivyo hakuna sababu ya mtu yoyote kupuuza maagizo haya,” alisema Bw. Mnyambwa.
Aidha, alifafanua kuwa mfumo wa NeST ni hatua ya kisasa iliyowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha mchakato wa manunuzi ya umma unakuwa wa haraka, wenye uwazi na unaozingatia ushindani wa haki kwa wazabuni wote.
“Napenda kusisitiza kwamba kuanzia sasa hakuna ununuzi wowote wa serikali utakaofanyika nje ya mfumo wa NeST. Hii ni sheria na maelekezo rasmi ya serikali. Yeyote atakayeenda kinyume na taratibu hizi atawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” aliongeza.
Mafunzo hayo ya siku tano yamekusudia kuwajengea uwezo Wakuu wa Idara, Wakuu wa Taasisi, Maafisa Ugavi, na wataalamu wengine kutoka Halmashauri zote za mkoa wa Njombe juu ya utekelezaji sahihi wa sheria ya manunuzi ya umma pamoja na matumizi ya mfumo wa NeST ili kuimarisha uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.