Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, jana asubuhi alishiriki zoezi la kupiga kura kwa kupiga kura yake katika mtaa wa Lunyanywi, ndani ya Halmashauri ya Mji wa Njombe. Akizungumza mara baada ya kupiga kura, Mhe. Mtaka amepongeza wananchi waliojitokeza mapema na kutoa wito kwa waliobaki kutumia muda uliosalia kutimiza haki yao ya kikatiba.
"Mkoa wa Njombe uko katika hali ya usalama, na mpaka sasa hatujapokea changamoto yoyote. Ninawasihi wananchi ambao bado hawajapiga kura wawahi ili kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi wao," alisema Mhe. Mtaka.
Wananchi wapatao 457,317, sawa na asilimia 86 ya waliosajiliwa, wanatarajiwa kushiriki uchaguzi huu muhimu wa Serikali za Mitaa, Vijiji, na Vitongoji katika mkoa wa Njombe. Kwa mujibu wa Mhe. Mtaka, ushiriki wa wananchi katika zoezi hili ni kielelezo cha uzalendo na uimara wa demokrasia nchini.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa amewahimiza wakazi wa Njombe kuendelea kudumisha amani na utulivu wakati wa uchaguzi, akisema: "Hii ni fursa ya kipekee kwa wananchi kuamua mustakabali wa maendeleo yao. Ni muhimu tushirikiane kwa amani na mshikamano."
Kwa ujumla, uchaguzi unaendelea kwa utulivu, huku vituo vya kupigia kura vikiripotiwa kuwa shwari na mazingira mazuri kwa wapiga kura. Wakazi waliojitokeza mapema wameridhishwa na hali ya utaratibu katika vituo vyao.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.