Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dodoma, Bw. Richard Kayombo, ameanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Njombe. Leo, amepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa, ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka.
Ziara hiyo inalenga kuwatembelea wafanyabiashara walipa kodi mkoani humo, kuwashukuru kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari, na kuwapongeza kwa mchango wao mkubwa uliowezesha TRA kuvuka malengo ya ukusanyaji kodi mkoani Njombe.
Akizungumza mara baada ya kusaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Bw. Kayombo aliwapongeza viongozi wa Mkoa wa Njombe kwa kushirikiana vizuri na TRA katika kuhakikisha mapato ya serikali yanakusanywa ipasavyo.
"Ninawashukuru viongozi wa mkoa huu kwa namna wanavyoshirikiana nasi. Ushirikiano huu umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuvuka malengo yetu ya ukusanyaji wa kodi mkoani Njombe," alisema Bw. Kayombo.
Bw. Kayombo aliongozana na Meneja wa TRA Mkoa wa Njombe, Bi. Spegoza Owure, katika ziara hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa, alimshukuru Mkurugenzi huyo kwa kutembelea mkoa huo na kuonyesha nia ya kuwatambua na kuwahamasisha walipa kodi.
"Kuwatambua walipa kodi na kuwashukuru ni jambo kubwa linalochangia kuwahamasisha zaidi. Tunaamini ziara yako itaongeza chachu kwa wafanyabiashara kuendelea kushiriki kikamilifu katika kulipa kodi," alisema Mhe. Gwakisa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe.
Ziara ya Mkurugenzi huyo inatarajiwa kuendelea kesho, akitembelea wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali mkoani Njombe.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.