Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) umeanzisha mpango maalum wa kugawa mitungi 13,020 ya gesi kwa bei nafuu katika wilaya nne za mkoa wa Njombe. Mpango huu unalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi, kuboresha afya za wananchi, na kutunza mazingira kwa kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 19 Novemba 2024 katika ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, kila wilaya itapokea mitungi 3,255 ambayo itauzwa kwa nusu bei ya kawaida, huku nusu nyingine ya gharama ikifidiwa na serikali. Mpango huu umeungwa mkono kwa karibu na kampuni ya Taifa Gas, ambayo imesaini mkataba wa usambazaji wa gesi kwa mwaka mmoja.
Akizungumza wakati wa kutambulisha mpango huu, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage, alisema lengo kuu ni kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi. “Kwa kawaida, gharama za gesi zimekuwa kikwazo kikubwa kwa kaya za kipato cha chini. Serikali imelipa nusu ya gharama ili kuhakikisha kila mwananchi anaweza kumudu,” alisema.
Mitungi itakayogawiwa ni ya ukubwa wa kilo sita, ambapo kila mtungi utauzwa kwa shilingi 19,500. Wananchi watatakiwa kuonyesha vitambulisho vya taifa kama njia ya kuthibitisha ustahiki wao wa kunufaika na mpango huu.
Mhandisi Mwijage aliongeza kuwa tathmini ya awali itafanyika baada ya usambazaji wa awamu ya kwanza ili kubaini kama wanufaika wanaendelea kutumia gesi, pamoja na changamoto zozote zinazoweza kuhitaji utatuzi.
Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, Mkuu wa Idara ya Miundombinu wa Mkoa, Mhandisi Rutashibilwa, alielezea umuhimu wa mpango huu katika mkoa wa Njombe. Alisema, “Njombe inakutana na changamoto kubwa ya matumizi ya kuni na mkaa, ambayo yanaathiri mazingira na afya za wananchi. Kupitia mpango huu, tunaamini tutapunguza athari hizi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.”
Aliendelea kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi ni muhimu ili kufanikisha malengo ya mradi. “Tunatoa wito kwa viongozi wa wilaya na vijiji kushirikiana na REA kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu faida za gesi kama mbadala wa nishati za kienyeji,” aliongeza.
Mpango wa REA wa kugawa mitungi ya gesi kwa bei nafuu unakuja wakati muafaka katika juhudi za kitaifa za kuhakikisha nishati safi inawafikia wananchi wa vijijini. Hii ni hatua muhimu ya kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kuboresha afya, na kulinda mazingira.
Wananchi wa Njombe wanahimizwa kuchangamkia fursa hii ya kipekee kwa kununua mitungi ya gesi na kubadili mtazamo kuhusu matumizi ya nishati salama na endelevu. Tujitokeze kwa wingi kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo!
ReplyForward Add reaction |
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.