Njombe – Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka madereva wa bodaboda na bajaji kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kuimarisha utaratibu wa matumizi ya barabara.
Akizungumza leo tarehe 12 Machi 2025 katika mkutano wa bodaboda uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Agrement mkoani Njombe, Mhe. Mtaka ameruhusu bodaboda na bajaji zote kutumia barabara zote ndani ya mji wa Njombe, kufuatia upanuzi wa miundombinu ya barabara unaoendelea kwa ufadhili wa serikali.
Agizo hilo limekuja baada ya madereva wa bajaji kuwasilisha malalamiko yao kuhusu kuzuiwa kutumia baadhi ya barabara kuu, jambo ambalo lilikuwa likiwaletea changamoto katika shughuli zao za kila siku. Kufuatia mjadala huo, Mkuu wa Mkoa aliagiza kuwa bodaboda na bajaji zote zitaruhusiwa kutumia barabara zote mjini, huku akisisitiza kuwa madereva wanapaswa kuheshimu sheria za usalama barabarani.
Aidha, Njombe inatarajia kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Jitihada zinaendelea ili kuanza kununua pikipiki za umeme kama sehemu ya mikakati ya kupunguza uchafuzi wa mazingira na gharama za mafuta.
Mhe. Mtaka aliwapongeza madereva wa bodaboda kwa kazi wanayoifanya katika kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi na kuwataka waendelee kutembea kifua mbele kwa kuwa kazi yao ni halali na yenye mchango mkubwa kwa jamii. Pia, aliwasihi wananchi na watumishi wa umma kuwaheshimu vijana hao kwani ni sehemu muhimu ya maendeleo ya mji wa Njombe.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.