Na Chrispin Kalinga Njombe, Tanzania
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Mhe. Prof. Adolf Mkenda amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi miwili muhimu ya maendeleo katika Mkoa wa Njombe ndani ya Halmashauri ya Wilaya wa Wanging`ombe ikiwemo mradi wa afya na mradi wa elimu. Ziara hii imelenga kutathmini hatua za utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo inalenga kuboresha ustawi wa wananchi na kuboresha huduma za kijamii katika mkoa huo.
Akianza ziara yake, Mhe. Mkenda amezindua Mradi wa Afya, ambao unahusisha ujenzi na Uboreshaji wa Miundombinu ya Kituo cha Afya cha Makoga ambapo Mradi huu umetekelezwa kwa gharama ya shilingi Milioni 500, ambayo imetolewa na serikali kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuweka miundombinu ya kisasa. Waziri alieleza kuwa ujenzi huo umekamilika ndani ya muda uliopangwa. Mhe. Waziri alipongeza juhudi za serikali kwa kuona umuhimu wa kuhakikisha kwamba vifaa vya kisasa vya matibabu vinawekwa ili kuboresha huduma za afya na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika vituo vya afya vya jirani.
Katika hatua ya pili ya ziara yake, Waziri ametembelea Mradi wa Elimu unaojumuisha ujenzi wa madarasa mapya katika Shule ya Sekondari ya Matapa, Mradi huu umegharimu shilingi Milioni 961.9 na fedha hiyo imetolewa na serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kukamilika kwa ujenzi huo umepunguza msongamano wa wanafunzi katika shule jilani na umewapunguzia wanafunzi umbali wa Kwenda kutafuta elimu zaidi ya kilomita tano. Mhe. Waziri wakati alipokuwa akiwasalimia wanafunzi wa shule hiyo Alisisitiza kuwa, elimu bora ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Wakati wa ziara hiyo, Waziri alitoa pongezi kwa wakazi wa Wanging`ombe kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa miradi hiyo, akibainisha kuwa mafanikio haya yanatokana na juhudi za pamoja kati ya serikali na wananchi.
Pia ziara hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali was serikali wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari na viongozi wa chama Cha mapinduzi Mkoa wa Njombe.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.