Njombe – Agosti 8, 2025
Mkoa wa Njombe unawatakia Watanzania wote Heri ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane), huku ukisisitiza nafasi yake ya kipekee katika sekta ya kilimo na kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji na usindikaji wa mazao.
Ujumbe huu unatolewa sambamba na maadhimisho ya Nane Nane mwaka huu, ambapo Mkoa wa Njombe umebainisha kuwa unajivunia uzalishaji wa mazao ya kimkakati ikiwemo parachichi, viazi mviringo, ngano, pamoja na fursa kubwa katika kilimo cha mazao mengine ya chakula na biashara. Kwa mujibu wa takwimu za kilimo, Njombe imekuwa ikipiga hatua kitaifa katika tija ya uzalishaji, huku miradi ya viwanda vya kuongeza thamani ikiendelea kujengwa ili kuhakikisha masoko ya uhakika kwa wakulima.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amesema kuwa hali ya hewa yenye baridi na rutuba ya ardhi inaufanya mkoa huo kuwa kitovu bora cha uwekezaji wa kilimo nchini. “Niwakaribisha sekta binafsi ambao watahitaji kufanya kilimo cha mazao ya chakula na biashara, niwakaribishe Njombe fursa hiyo ipo,” alisema Mhe. Mtaka. Aidha, amesisitiza kuwa uwepo wa viwanda vipya vya parachichi ni suluhisho la kudumu kwa changamoto za masoko kwa wakulima.
Kwa ujumla, Mkoa wa Njombe utaendelea kushirikiana na wawekezaji, wakulima, na wadau wote wa kilimo kuhakikisha sekta hii inakuwa kichocheo kikuu cha uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
KARIBU NJOMBE
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.