Njombe, 11 Agosti 2025 – Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Njombe leo kimefanya kikao chake cha kikatiba ambapo pamoja na mambo mengine kimepitia utekelezaji wa mipango na taarifa za vikao vilivyopita.
Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Njombe, Dr. Mashaka Kisulila, na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka halmashauri zote za mkoa huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Dr. Kisulila alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutekeleza kwa vitendo ombi la watumishi wa umma la nyongeza ya mishahara, ambapo utekelezaji huo umeanza rasmi mwezi Julai mwaka huu.
"Rais wetu ametusikiliza, ametujibu na ametutendea kwa vitendo. Kwa niaba ya watumishi wote wa Mkoa wa Njombe, tunasema asante sana Mhe. Rais kwa kutuongezea mshahara na kuthamini mchango wetu. Tunakuahidi tutaendelea kuunga mkono jitihada zako kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa," alisema Dr. Kisulila.
Aidha, aliwataka watumishi wa umma wote kutumia fursa ya nyongeza ya mishahara kuongeza bidii na weredi kazini, huku wakionyesha hamasa ya hali ya juu katika kutimiza majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, sasa mtumishi wa kimo cha chini hulipwa kuanzia shilingi laki tano (500,000), hatua inayochangia kuinua maisha na ustawi wa watumishi wa umma nchini.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.