Vijiji saba ilivyopo katika mgogoro wa mpaka kati ya wilaya za Makete na Wanging'ombe mkoani Njombe,ambavyo vilipimwa wakati wa ugawaji wa wilaya vimeagizwa virudiwe kupimwa upya.
Agizo hilo lilitolewa na waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Jerry Silaa wakati wa ziara yake mkoani hapa alisema kwa sababu mchakato wa upimaji uliotumika hapo awali haukuzingatia tangazo la serikali la upimaji wa mipaka.
Agizo hilo limekuja kufuatia timu ya wapimaji wa ramani kutoka wizara ya ardhi kufika na kufanya tafsiri ya tangazo la serikali lililotumika kuanzishwa kwa wilaya ya Makete na Wanging'ombe.
‘’Mipaka ya vijiji vyote vilivyopimwa irudiwe kupimwa upya kwa kuzingatia matangazo ya mipaka ya wilaya kwa kuwa upimaji wa mwanzo haukuzingatia mipaka ya matangazo ya serikali,’’alisema Silaa.
Pia waziri alisema pendekezo la pili wananchi wa pande zote mbili waheshimu mpaka wa wilaya hizo kulingana na tafsiri ya matangazo ya serikali ya mipaka kama yalivyotafsiriwa na timu ya wataalamu.
Waziri Silaa alisema migogoro ya mipaka isiwaingize viongozi kwenye malumbano ambayo hayasaidii.
‘’Lakini kubwa ni yale maelezo yote hasa lile nililosema la kupima upya vijiji,nikimuandikia taarifa yangu mh makamu wa Rais(Dk.Philip Mpango)naamini litafanyika kwa haraka kwa sababu tunaenda kwenye mwaka wa uchaguzi wa vijiji na vitongoji na mitaa kwa hiyo kila mtu ajitambue kuwa yuko wapi,’’alisema Silaa.
Awali wawakilishi wa wananchi kutoka katika vijiji vya kata ya Moronga wilaya ya Makete pamoja na wanaotoka katika vijiji vinavyounda kata ya Kipengere wilaya ya wanging'ombe walisema kilichokuwa kinasumbua miaka yote ni mkanganyiko kwenye ramani.
‘’Kwenye ramani kinasoma kingine,kwenye gazeti la serikali kinasoma kingine,mkienda kwenye ardhi mnaonyeshwa mahali pengine ,’’alisema Ebrania Mbilinyi.
Katibu Tawala mkoa wa Njombe Bi.Judica Omari alisema serikali imetoa fedha nyingi ili kufanikisha zoezi la upimaji wa ardhi.
Waziri pia alifika kusikiliza mgogoro wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania Dayosisi ya Kusini na wakazi wa mtaa wa Lunyanywi na Magoda ambapo aliiagiza timu ya wataalamu kutoka wizara ya ardhi kufika na kufanya kazi ili kubaini ukweli.
‘’Na timu ikija itaongea na kila mtu mmoja mmoja,pia naagiza ujenzi usimame kwa sababu ni eneo la mgogoro mtu uwa anajenga sehemu yake,na sehemu hii kanisa linasema ya kwake na nyie mnasema ya kwenu,naahidi kurudi tena januari 2024 ili kumaliza mgogoro huu’’alisema Silaa.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.