Njombe, 22 Machi 2025 – Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amehitimisha ziara yake katika Wilaya ya Wanging’ombe baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kuhutubia wananchi katika mikutano ya hadhara iliyofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Ilovi-Makoga na baadaye katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Igwachanya.
Akiwahutubia wananchi katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ilovi-Makoga, Mhe. Majaliwa aliipongeza Wilaya ya Wanging’ombe kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa miradi hiyo ili kuhakikisha inawanufaisha kwa muda mrefu. Aidha, aliwakumbusha wazazi na walezi umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata elimu, akisisitiza kuwa hilo si hiari bali ni wajibu wa kila mzazi.
Baada ya mkutano huo, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Itulahumba hadi Igwachanya yenye urefu wa kilomita 19.25. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 86 na unatarajiwa kukamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 9.8. Mhe. Majaliwa alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara ili kuboresha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Njombe.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Igwachanya, ambapo Waziri Mkuu alizungumzia uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika sekta ya elimu. Akitolea mfano Shule ya Sekondari ya Mkoa ya Wasichana ya Njombe, iliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4, Mhe. Majaliwa aliwataka wanafunzi wote kuzingatia masomo na kuonesha mshikamano kwa wenzao wenye mahitaji maalum. Katika hotuba yake ya kumaliza ziara, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo mkoani humo, akibainisha kuwa juhudi hizo zinaakisi dhamira ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.