Njombe, 23 Machi 2025 – Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, leo amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe, ambapo amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kuhusu juhudi za serikali katika kukuza uchumi wa viwanda.
Akiwa katika siku yake ya mwisho ya ziara, Mhe. Majaliwa alihutubia wananchi wa Makambako kwenye mkutano wa hadhara, akiwahimiza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kuitumia fursa ya kilimo cha parachichi kuinua uchumi wao.
Baada ya mkutano huo, alitembelea Kiwanda cha Kusindika Parachichi cha AVOAFRICA, kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, ambacho kinaendelea kuongeza thamani ya zao la parachichi kwa ajili ya soko la ndani na la kimataifa. Katika ziara hiyo, alisifu juhudi za wawekezaji na kuhimiza uendelezaji wa viwanda vya kusindika mazao mengine ya kilimo.
Aidha, Mhe. Majaliwa alitembelea Kiwanda cha Kuchuja Mafuta ya Parachichi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, ambapo alieleza kuwa uwekezaji huo ni hatua muhimu katika kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa Njombe.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, kwa jitihada kubwa za kupanua wigo wa uchumi wa viwanda mkoani humo.
"Njombe inakuwa mfano mzuri wa uchumi wa viwanda. Tayari tunaona Kiwanda cha Kusindika Parachichi kinafanya kazi, Kiwanda cha Kuchuja Mafuta ya Parachichi nacho kinaendelea na uzalishaji, na bado kuna viwanda vingine vinajengwa hapa hapa Njombe. Tunashuhudia pia ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Chuma na Kuunda Magari. Hili ni jambo la kupongeza sana. Hongera sana Mkuu wa Mkoa kwa kazi nzuri ya kuvutia uwekezaji na kufanikisha mapinduzi ya viwanda hapa Njombe,” alisema Mhe. Majaliwa.
Ziara ya Waziri Mkuu mkoani Njombe ilikuwa na lengo la kukagua miradi ya maendeleo, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchumi wa viwanda, na kuhakikisha rasilimali za mkoa zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi wote.
Mwisho.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.