SERIKALI mkoani Njombe imesema haitawavumilia hata kidogo na badala yake itawachukulia hatua kali za kisheria wafanyabiashara wote watakaobainika kuwauzia mbolea feki kwa wakulima.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Njombe Mh. Antony Mtaka,wakati akizungumza na waumini wa Kanisa la Waadvetista Wasabato ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya sikukuu ya Makambi yanayofanyika viwanja vya sabasaba mjini hapa.
"Muwashauri wafanyabiashara wa mbolea nyinyi wazawa wa Njombe wasiingie kwenye kuwauzia mbolea feki,serikali inamkono mrefu,jicho la serikali liko kila mahala tusije tukalaumiana kwa mtu aliyeuza mbolea feki hatutakua na msamaha wa aina yeyote"alisema Mtaka.
Mtaka alibainisha kuwa"Tumeambiwa na wenzetu wa hali ya hewa mwezi wa kumi mvua zitaanza mvua kubwa,niwaombe wananchi ambao wanashughulika na mambo ya kilimo waandae mashamba,tutaleta mbolea ya ruzuku mapema,tutaleta mbegu kwenye maduka mapema,nunua mbolea yako vizuri"alisema.
Mtaka aliwataka wananchi mkoani humo kutafuta njia bora ya kutatua migogoro na sio kuuwana kwa sababu visasi kwenye familia na biashara ni sababu kubwa zinazochangia kuwepo kwa matukio hayo.
"Niwaombe tujiepushe na kulipizana visasi,kama mashamba ya miti umeambiwa kwamba baba yako alipofariki mama yako aliachiwa miti akadhulumiwa na mashemeji zake tafuta namna nzuri ya kupata haki ya miti ya baba yako,usiende kuichoma wala usiende kukodisha watu kwa ajili ya kwenda kumuua baba mdogo wala mjomba"alisema Mtaka.
Alitoa rai kwa wafanyabiashara wa sokoni hapo kujiepusha na mikopo umiza na badala yake wafanye biashara kwa kuzingatia misingi mizuri ili waweze kukuza biashara zao
Hata hivyo aliwataka wanafunzi wanaojiandaa na mitihani kidato cha pili na cha nne kwamba ili wafaulu wanapaswa kusoma kwa bidiii na si vyenginevyo.
"Hakuna muujiza,kama kuna mapepo ya kukemea,kemea mapepo ya kuwa mjinga wa kusikiliza maubili ambayo hayana kichwa wala miguu,kama kuna mapepo ya kukemea tukemee mapepo ya uvivu ili tusome kwa bidii,tufanye kazi kwa bidii"alisema Mtaka.
Awali katibu mkuu NGDF ambaye pia ni mnenaji mkuu wa Makambi,mchungaji Richard Mashauri kutoka wilayani Kahama mkoani Shinyanga alisema waumini wanapaswa kupinga mauaji ya vikongwe,watoto,ushonga na utajiri kwa njia ya miujiza.
"Hakuna utajiri kwenye biblia unaosema paka mafuta ya upako,hakuna ndani ya biblia unaosema ua kikongwe utajirike haupo,utajiri unatokea kwa nguvu binafsi za mtu kwa kufanya kazi"alisema Mashauri.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.