Wanawake kutoka makundi mbalimbali wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, wamekabidhi misaada ya kibinadamu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Msingi na Sekondari Viziwi Njombe. Misaada hiyo ni pamoja na mavazi, vyakula, taulo za kike, na fedha taslimu kiasi cha Shilingi milioni moja. Shule hiyo inakabiliwa na changamoto za uendeshaji baada ya kuondoka kwa wafadhili waliokuwa wakiiunga mkono.
Akizungumzia sababu ya kusaidia shule hiyo kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Bi. Judica Omari, akishirikiana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Njombe, Bi. Anna Mwalongo, amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, hususan za kifedha. Wamesema msaada huo utasaidia kupunguza ugumu wa maisha kwa wanafunzi hao na kuwa chachu ya mabadiliko chanya.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Mchungaji Alphonce Ngavatula, pamoja na wanufaika wa msaada huo, wamewashukuru wanawake hao kwa kuguswa na hali yao. Aidha, wameahidi kutumia misaada waliyopewa kwa uangalifu na kwa manufaa ya wanafunzi.
Mbali na kutoa misaada, wanawake hao pia walipanda miti ya parachichi ili kuboresha afya, mazingira na uchumi wa shule hiyo. Pia, walitembelea miradi ya kilimo cha kitaru nyumba inayojumuisha uzalishaji wa nyanya na pilipili hoho kama sehemu ya kuhamasisha maendeleo ya kilimo miongoni mwa wanafunzi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.