WANANCHI WA HALMASHAURI YA MJI WA MAKAMBAKO MKOANI NJOMBE WASEMA MH.RAIS DKT.JOHN MAGUFULI ASIENDE KUOMBA KURA MWAKA 2020,NA BADALA YAKE AENDE KUSHUKURU MWAKA 2021.
WANANCHI wa Kata ya Mlowa, Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe wamemtaka Rais Dk. John Magufuli asiende katika Jimbo la Makambako linaloongozwa na Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Deo Sanga kwenda kuomba kura mwaka 2020 katika uchaguzi Mkuu na badala yake aende mwaka 2021 kushukuru,kwa kura za kishindo watakazomchagua.
Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa jimbo hilo mheshimiwa Deo Sanga wakati akimweleza Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Mzee Mkongea Ali alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Halmashauri ya Mji wa Makambako ambayo imeelezwa imekuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Makambako itakayosaidia kuondoa changamoto ya huduma za matibabu.
"Kiongozi wa mbio za Mwenge nakupa ujumbe wa wananchi wa Kata ya Mlowa nilipofanya mkutano hapa walinieleza nifikishe ujumbe kwa Rais, na Mimi nakuomba ufikishe salam zao kwa mheshimiwa Rais,kwamba wanaomba mwaka 2020 asije kwenye jimbo letu la Makambako kuomba kura," alisema Sanga.
Ameongeza kusema kuwa wananchi wa Kata ya Mlowa wanaishukuru serikali kwa kuongeza pesa kiasi cha shilingi Milioni Mia tano na hivyo jumla ya pesa zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo Saba ya hospitali hiyo kuwa ni Shilingi bilioni mbili.
"Rais Magufuli ametuongezea Shilingi milioni mia tano tulipokuwa tumeomba ili kukamilisha hospitali yetu, tunamshukuru sana Mheshimiwa kwa kukubali ombi letu," amesisitiza.
Mbio za Mwenge zimeanza rasmi kukimbizwa mkoani hapa Septemba 15, mwaka huu ambapo Mkuu wa mkoa wa Njombe,Mheshimiwa Christopher Ole Sendeka akipokea Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji wa Makambako kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Iringa, Ali Happi ambapo amesema jumla ya miradi 54 yenye thamani ya shilingi bilioni 34 itapitiwa na mbio za Mwenge katika wilaya zote nne za mkoa wa Njombe.
Aidha mheshimiwa Sendeka ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Pombe Magufuli kutatua changamoto mbalimbali hususani katika sekta ya barabara na afya.
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi wa Kata ya Mlowa, Halmashauri ya Mji Makambako wameshuhudia kiongozi wa mbio za Mwenge akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya jambo ambalo wamesema wanatarajia kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma za matibabu zitakuwa zimekwisha wakati hospitali hiyo itakapoanza kutoa huduma za matibabu. "Tunafurahi Mwenge wa Uhuru kupitia hapa kwenye ujenzi wa hospitali hii ya Halmashauri, itatusaidia kuondoa tatizo lililokuwepo la muda mrefu la sisi wanawake kutembea umbali mrefu kufuata matibabu," alisema Juliana Mligo”
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.