Wakazi wa Halmashauri ya mji Njombe wameendelea kupata huduma mbalimbali za Kibingwa na Bobezi kupitia Mpango Kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini katika Afya ya Msingi.
Mpango huo wenye lengo la kusogeza huduma za Kibingwa karibu na wananchi pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya ya msingi, umeingia katika siku yake ya Pili leo Mei 7 hapa katika Hospitali ya Halmashauri ya mji Njombe (Kibena) ikishuhudiwa huduma mbalimbali zikitolewa kwa wanufaika ikiwemo huduma za Kibingwa za Magonjwa ya Ndani, Upasuaji, Huduma za Bobezi za watoto wachanga, Huduma za Kibingwa za Magonjwa ya wanawake na uzazi, pamoja na uwepo wataalamu wa huduma Ganzi na Usingizi.
Miongoni mwa wananchi walionufaika na huduma hizo za Kibingwa ni Grace Fungo, Mkazi wa Njombe, ambaye ameishukuru serikali kupitia Mhe. Rais kwa kuanzisha program hiyo ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi ambao walihitaji kupata huduma hizo katika hospitali kubwa zaidi kama vile Muhimbili.
Akizungumza mapema leo Dkt. Ernestina Mwipopo Daktari Bingwa Mbobezi katika magonjwa ya watoto wachanga, akiwa pia ni msimamizi wa Jopo hilo la Madaktari Bingwa kwa Halmashauri ya mji Njombe, amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi katika kupima na kupata matibabu katika Hospitali hiyo.
Hapo jana akizindua mpango huo Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alisema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepunguza idadi ya vifo vya akinamama wajawazito kwa asilimia 80, kutoka katika vifo 556 kati ya vizazi hai 100000 hadi vifo 104, kati ya vizazi hai 100000
Mpango huo kabambe unatarajiwa kufikia tamati mnamo Juni 28 mwaka huu kwa nchi nzima, huku kwa Mkoa wa Njombe ukitarajiwa kufanyika kwa siku tano, kuanzia hapo jana Mei 6 hadi Mei 10, 2024.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.