WANANCHI WA KATA YA WANGING'OMBE MKOANI NJOMBE WATAKIWA KUTUMIA VITUO VYA AFYA,HOSPITALI KUPATA TIBA SAHIHI,SANJARI NA MRADI WA MAJI WA KATA YA ILEMBULA KUONDOA KERO YA MAJI PINDI UTAKAPOKAMILIKA
Wananchi wa kata ya wanging'ombe mkoani Njombe wamehimizwa kuacha hurka ya kukimbilia kutumia tiba za miti shamba na nyinginezo na badala yake watumie fursa ya uwepo wa hospitali na vituo vya Afya zaidi ya 300 vilivyojengwa nchini na serikali ya awamu ya tano kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wameunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli.
Rai hiyo imetolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Mzee Mkongea Ali wakati akiweka jiwe la msingi la majengo ya maabara, wodi ya wazazi, nyumba ya mtumishi pamoja na ofisi ya kuhifadhia taarifa muhimu za mahesabu zilizojengwa kutokana na fedha zilzilizotolewa na serikali zaidi ya shilingi Milioni 400.
"Na wasihi wananchi tutumie hospitali na vituo vya Afya vilivyojengwa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli ili kumuunga mkono kwa kufuata huduma za matibabu za kitaalam kupitia wataalam waliosomea badala ya kukimbilia tiba mbadala isiyokuwa pengine bora," alisema Ali.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya,Francis Hoya alisema kuanza kutumika kwa majengo yaliyoanza kutoa huduma mbalimbali za matibabu kumepelekea kutoa huduma za upasuaji wa uzazi kwa wanawake 30.
"Kuwepo kwa utoaji wa huduma mbalimbali za Afya kwenye kituo hiki kimekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi na kuondoa tatizo la kufuata matibabu katika hospitali nyingine hapa wilayani," alisema Hoya.
Katika hatua nyingine, Mbio za Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Kata ya Wanging'ombe na Ilembula uliweka jiwe la msingi katika mabweni ya wanafunzi wasichana na wavulana wa shule ya Sekondari Wanging'ombe, huku kiongozi wa mbio za mwenge akiacha kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa tanki la maji la mradi uliogharimu zaidi ya shilingi Milioni 300 kutokana na mapungufu ya kiuhandisi .
Awali mkuu wa wilaya hiyo Ally Kasinge amesema kujengwa kwa mradi huo kutasaidia upatikanaji wa maji katika Kata ya Ilembula wilayani Wanging'ombe,na kuahidi kuyatafutia ufumbuzi mapungufu yote yaliyojitokeza ambapo unasimamiwa na mamlaka ya maji Wanging'ombe (Wangiwasa).
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.