Wafanyakazi wa Kiwanda cha Chai Kibena Kilichopo Wilaya ya Njombe, waliokuwa wamegoma kwa siku 5 wamerejea kazini mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka kufanya ziara Julai 5, 2024 katika kiwanda hicho cha Chai kinacho simamiwa na Kampuni ya DL Group ambapo Mhe. Mtaka aliitaka Kampuni hiyo kuanza kulipa mishahara yao zaidi ya milioni 200 na Mishahara hiyo ilianza kulipa muda huo huo.
Mkurugenzi wa Makampuni ya DL Group Tanzania, Jamerson Moturi alisema ni kweli wafanya kazi hao hawajalipwa mishahara yao kwa kipindi cha miezi minne na aliahidi mbele ya Viongozi wote waliohudhulia Mkutano huo wa Mkuu wa Mkoa kuwa mpaka mwishoni mwa mwezi Agosti atakuwa amemaliza malimbikizi yote ya Mishahara ya wafanyakazi hao.
“Leo julai tano tunalipa mshahara mmoja ambao ni shilingi milioni 200.1 na wiki ijayo Julai 11 tunalipa mshahara mwingine wa miezi miwili shilingi milioni 400 na mwezi Agosti tarehe nane tutalipa mshahara mwingine na kukamilisha,” alisema Moturi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka alisema jambo la kutokulipwa mshahara wafanyakazi hao linafedhehesha kwa sababu mshahara ni kipato kinachosaidia wao kufanya shughuli zao.
“Mnaendesha maisha, mnapeleka watoto shule, mnajitibia lakini mambo mengine yanaenda bila ya kuwa ombaomba,” alisema Mhe. Mtaka
Wafanyakazi wa kiwanda hicho walisema wanaishukuru serikali kwa kuingilia kati suala hilo na hivi sasa wapo tayari kuingia kazini kwa sababu wanauhakika wa kulipwa mishahara yao.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.