ASASI ya kilele inayoshughulisha na kilimo cha mbogamboga, matunda na mimea itokanayo na mizizi na viungo Tanzania Horticultural Association (TAHA) wamekabidhi vyeti vya hithibati kwa wakulima wapatao 300 wa Parachichi waliokidhi viwango vya kimataifa kufikia soko Barani Ulaya.
Hayo yamelezwa na Mratibu wa Maendeleo Biashara kutoka TAHA, Asia Barnabas mara baada ya Mkutano wa jukwaa la wadau wa Parachichi uliofanyika mkoani hapa.
Barnabas alisema malengo ni kuhakikisha parachichi inayolimwa Tanzania inafikia masoko makubwa duniani.
“Na ili parachichi iweze kufikia masoko inatakiwa ianze kuwa na ubora kuanzia inapozalishwa, lakini tunaiomba sasa serikali yetu ya mkoa na serikali kuu kuhakikisha hizi changamoto ya kimiundombinu zinazosababisha parachichi hii pendwa isifikie mlaji au isifikie soko ziangaliwe,” alisema Barnabas.
Hata hivyo Barnabas amesema hakuna namna ya kufikia soko la dunia bila ya kuhakikisha kwamba changamoto zenye uzito mkubwa kwa wakulima na wafanyabiashara zinatatuliwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka aliwaagiza Wakala wa barabara Mjini na Vijijini (TARURA), Shirika la umeme (TANESCO) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha kila taasisi inatatua changamoto katika eneo lake.
“Muanze mara moja mpango wa kujenga barabara zinazoelekea maeneo ya uwekezaji mkubwa, pia mnatakiwa kusogeza huduma ya umeme ili utumike kwa umwagiliaji mashambani na ushimbaji wa visima virefu kwa mkulima mmoja mmoja,” alisema Mtaka.
Mtaka amesema kuwa kabla ya kufikia hatua za kuchukua ushuru kwa wakulima ni vyema sasa huduma hizo zikaboreshwa ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na ubora unaotakiwa katika soko la dunia.
Mmoja wa wakulima hao, akiwemo Edger Mtitu alisema endapo mkakati wa kilimo na masoko uliyowekwa na serikali utafuatwa utaleta mageuzi katika uzalishaji pamoja na uchumi.
Pia ameomba serikali kudhibiti makampuni ambayo yananunua mazao ikiwemo parachichi Mkoa wa Njombe na kuyagonga nembo za Mataifa mengine hali ambayo inasababisha kuondoa uhalisia wa zao husika.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.