UMEME WA ACRA-LUGARAWA MEGAWATI 1.7 KUNUFAISHA WANANCHI WA VIJIJI ISHIRINI KATIKA UCHUMI WA VIWANDA WILAYA YA LUDEWA MKOANI NJOMBE
WANANCHI wa Kata ya Lugarawa, Wilayani Ludewa Mkoani Njombe wameipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kwa hatua ya kuwaletea umeme wa maji unaofadhiliwa na shirika la ACRA utakaowezesha upatikanaji wa umeme wa kilowati 1700 ambao ni sawa megawati 1.7.
Kati ya umeme huo, megawati 0.7 zitatumiwa na kata sita zilizopo kwenye wilaya ya Ludewa na kuhudumia wananchi wanaoishi katika vijiji 20.
Hayo yamesemwa na msoma risala wa mradi huo ambae ni Afisa maendeleo ya jamii wa kata ya lugarawa Oresta Mkalawa wakati mbio za mwenge wa uhuru zilipokwenda kuweka jiwe la msingi katika mradi huo wa umeme unaozalisha nishati ya umeme kwa kutegwa kwa bwawa kubwa lililopo juu yam lima kutokana na vyanzo mbalimbali vya maji ya chemichem vinavyopatikana kwenye kata hiyo.
Mradi huo ulioanza kujengwa tangu mwaka 2014 chini ya usimamizi wa shirika la ACRA ikishirikiana na kanisa Katoliki Jimbo la Njombe na kampuni ya Studio Frosio ya nchini Italia utazinduliwa mwezi Oktoba mwaka huu ukiwa umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 19.8.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia mradi huo akiwemo Bosco Mgimba ambaye ni mkazi wa kata ya Lugarawa amesema “wanashukuru sana kwa mradi huu utatunufaisha katika mambo mengi kama vile kwa kuwa mwanzoni matumizi tuliyokuwa tukiyatumia ndani ya nyumba ni kuwasha mishumaa ndani ya nyumba, vibatali na hata kutumia mafuta ya taa, lakini kwa ujio wa mradi huu tutaweza kuanzisha viwanda vyetu vidogo,” amesema Bosco Mgimba.
Oresta Mkalawa ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Lugarawa amesema jumla ya wajisiamali wadogo na wakati 340 watanufaika katika mradi huo na kati yao 40 watasaidiwa na shirika la ACRA kwa kununuliwa vifaa vya kuanzisha viwanda pamoja na mafunzo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere amesema wilaya ya Ludewa wapo wananchi wenye ujuzi na maarifa wakutaka kusukuma gurudumu la maendeleo ya kiuchumi ili kuitikia rai ya serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda, lakini kwa kipindi kirefu kikwazo cha kufikia lengo lao kwenye maeneo ya vijijini ilikuwa ni kukosekana kwa nishati ya umeme ambayo ingekuwa msaada wa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.
Mradi huo wa umeme wa maji uliopitiwa na Mwenge wa Uhuru na kuwekwa jiwe la msingi baada ya kupongezwa na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Mkongea Ali,ambapo amesema ni vyema wananchi wakaichangamkia fursa ya upatakinaji wa nishati hiyo ya umeme ili kuweza kubadilisha maisha yao kiuchumi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.