Kwa mara nyingine tena, Tanzania inakaribia kuandika historia kupitia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024. Hii ni nafasi ya kipekee kwa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wa mitaa, vijiji, na vitongoji ambao watawakilisha masilahi yao na kusimamia maendeleo katika maeneo yao.
Katika hatua za maandalizi, mikutano ya kuwanadi wagombea wa nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa tayari imezinduliwa jana tarehe 20 Novemba 2024, na itaendelea hadi tarehe 26 Novemba 2024. Kwa Mkoa wa Njombe, vyama vya kisiasa vinaendelea kuwanadi wagombea wao katika maeneo mbalimbali, huku wakiweka msisitizo kwenye mipango ya maendeleo inayolenga kuimarisha maisha ya wananchi.
Kusimamia Maendeleo ya Jamii:
Viongozi wa Serikali za Mitaa wanahusika moja kwa moja na mipango ya maendeleo kama vile huduma za afya, elimu, usafi wa mazingira, na miundombinu. Kupiga kura kunahakikisha unapata viongozi wanaojali mahitaji ya jamii yako na wanaosimamia rasilimali kwa uadilifu.
Kutumia Haki Yako:
Haki ya kupiga kura ni mojawapo ya alama kuu za uhuru wa raia. Usiposhiriki, unakosa fursa ya kushawishi maamuzi muhimu yanayogusa maisha yako na ya kizazi kijacho.
Kuimarisha Demokrasia:
Ushiriki wa wananchi kwa wingi katika uchaguzi unaimarisha misingi ya demokrasia. Ni uthibitisho kwamba watu wanaheshimu na kuzingatia mchakato wa kidemokrasia katika uongozi wa nchi.
Ili kushiriki kikamilifu tarehe 27 Novemba 2024, hakikisha kuwa wewe uliyejiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura. Tambua eneo lako la kupigia kura na ujue wagombea wote ili kufanya uamuzi wa busara.
Katika mikutano ya kampeni inayoendelea, hakikisha unafuatilia sera na ahadi za wagombea mbalimbali. Tambua nani ana maono yanayolingana na mahitaji ya jamii yako na uchague kwa hekima.
Tunaelekea kwenye siku muhimu katika historia ya taifa letu. Hakuna sababu ya kusubiri. Hakuna sababu ya kususia. Hakuna sababu ya kusema kura moja haiwezi kuleta mabadiliko. Kwa sababu kura yako inaweza kuwa ya kuamua mshindi!
Njoo, piga kura, na hakikisha sauti yako inasikika. Novemba 27, 2024, ni siku yako ya kufanya mabadiliko. Tukutane kwenye vituo vya kupigia kura na tuonyeshe uzalendo wetu kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Tanzania ni yetu sote. Tuitunze kupitia viongozi bora.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.