Njombe, Julai 24, 2025 – Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imekabidhi dawa muhimu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 6 kwa Gereza la Wilaya ya Njombe, ikiwa ni hatua ya kuimarisha huduma za afya kwa wafungwa na mahabusu walioko katika gereza hilo.
Dawa hizo zimekabidhiwa na Meneja wa TMDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Anitha Swai Mshighati, na kupokelewa na Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Njombe, SSP Jamhuri Y. Njaidi, katika hafla fupi iliyofanyika gerezani hapo mapema leo. Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, SSP Jamhuri ameishukuru TMDA kwa kuona umuhimu wa kusaidia afya za mahabusu na wafungwa wanaokutana na changamoto mbalimbali za kiafya.
Bi. Anitha Swai amesema kuwa dawa hizo ni sehemu ya dawa ambazo zilipatikana katika maduka ya dawa yaliyokuwa yakihifadhi na kuuza dawa ambazo haziruhusiwi kisheria katika maduka hayo, kwa kuwa dawa hizo zinatakiwa kutolewa katika zahanati na vituo vya afya pekee. Alibainisha kuwa TMDA imeamua kuzielekeza dawa hizo kwenye taasisi zinazohitaji msaada wa huduma za afya kwa dharura.
Aidha, meneja huyo ametoa wito kwa wamiliki wote wa maduka ya dawa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kufuata miongozo na sheria za usambazaji na uuzaji wa dawa. Amesisitiza kuwa TMDA itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa dawa zinatolewa na kutumika katika maeneo sahihi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Hatua hiyo ya TMDA imeelezwa kuwa ni ya kipekee katika kuhakikisha kuwa hata wale walioko katika mazingira magumu kama gerezani, wanapata haki ya msingi ya huduma ya afya, huku ikionesha dhamira ya mamlaka hiyo katika kusimamia usalama wa dawa nchini.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.